Tuifuate Njia ya Msalaba, tuifuate mpaka Kalvari Tusimamapo bila haya, msalaba msalaba huponya roho
Umekosa Nini we Yesu, kushtakiwa bure kwa Pilato Wenye kustahili hukumu, si wewe, si wewe, Bwana ni sisi
Ole msalaba huo mzito, apagazwa Mwana Mpenzi wa Mungu Mwili waenea mateso, alipa, alipa madhambi yetu
Ona Mumba Mbingu na nchi, yupo chini mzigo wamwelemea Na mtu kiumbe chake kwa ukali, ampiga, ampiga bila huruma
Huko njiani we Maria, waonaje hali ya mwanao Ni damu tupu na vidonda, machozi, machozi yamfumba macho
Kwa Simoni heri ya kweli, mimi pia Yesu nisaidie Kuchukua mzigo wa ukombozi, kuteswa, kuteswa pamoja nawe
Uso wa Yesu malaika, Bethlehemu wakuabudu Bahati yake Veronika, kupangusa, kupangusa mfalme wa mbingu
Wakimvuta huku na huku, wauaji wakamchokesha bure Chini wamtupa bado kwa nguvu, aibu, aibu yao milele
Wanawake wa Israeli, msilie kwa sababu hiyo Muwalilie hao kwa dhambi, upanga, upanga ni juu yao
Mwokozi sasa ni ya tatu, kuanguka chini ya msalaba Katika dhambi za ulegevu, nijue, nijue kutubu hima
Muje malaika wa Mbingu, funikeni mwiliwe kwa huruma Vidonda vyake na utupu, askari, askari wamvulia
Hapo mkristu ushike moyo, Bwana wako alazwa msalabani Mara miguu na mikono, yafungwa, yafungwa kwa misumari
Yesu mpenzi nakuabudu, msalabani unapohangaika Nchi yatetemeka kwa hofu, na jua, na jua linafifia
Mama Maria mtakatifu, upokee maiti ya mwanao Tumemwua kwa dhambi zetu, twatubu, twatubu kwake na kwako
Pamoja naye kaburini, zika dhambi na ubaya wa moyo Yesu tuwe wakristu wa kweli, twakupa, twakupa sasa mapendo
Katika roho yangu Bwana, chora mateso niliyokutesa Nisiyasahau madeni, na kazi, na kazi ya kuokoa
top of page
bottom of page
Comments