WAWILI WATAKUWA MWILI MMOJA
Nikitizama katika pango namuona mtoto Yesu. Katika yeye namuona Mungu aliyetumiminia ukarimu wake. Lakini nikijitazama mimi mwenyewe ninaona aibu kwa sababu ni kama naona katika mwili wangu moyo wa mtoto mdogo katika mwili wa mtu mzima. Katika mtoto Yesu namuona Mungu aliyejinyenyekeza na kutwaa hali ya kibinadamu. Lakini mimi nimekuwa kama debe tupu ambalo haliachi kuvuma. Ninamuona Maria ni mzuri kulingana na wema uliopo katika moyo wake. Uzuri wa sura pasipokuwa na wema, uzuri huo hauna maana. Namuona Yosefu, ni mkimya hata kama Maria yupo karibu naye. Wote wamejiweka kwa Mungu aliye katika hori la kulishia ng’ombe. Ulimwengu wetu unamchukulia mtu aliye mkimya kama ana mapungufu. Ndio maana baadhi ya redio zinatufanya tushindwe kulala usiku kucha zikiwa zinapiga nyimbo ile maarufu ‘Silent night.’ Nikitazama katika pango, namsikia Maria akimwambia Yosefu kwamba watu wanazungumza vibaya kutuhusu. Kwamba tumepata mtoto kabla hatujaishi pamoja. Yosefu anamwambia usihofu Maria, hofu haisaidii chochote. Katika sherehe ya Noeli tunasherehekea mambo mengi, na moja kati ya hayo ni ndoa. Tunapozungumzia ndoa, Maandiko Matakatifu yanatuambia kwamba wawili wanakuwa mwili mmoja. Jambo hili ni la kweli katika namna mbali mbali, na hili linajitokeza katika muujiza wa kuzaliwa. Mtoto anazaliwa kutokana na upendo uliopo kati ya baba na mama. Wazazi hawa wanaleta matumaini mapya, na furaha.
Katika sherehe hizi tunasherehekea ndoa. Sio ndoa kati ya wanadamu wawili, bali ni ndoa kati ya Mungu na sisi. Ndoa kati ya mbingu na nchi. Na katika hilo tunapata maisha mapya, na kuleta furaha katika ulimwengu uliopoteza mwelekeo. Mtoto anapozaliwa katika familia kwa hakika tunafurahi, na tunashangilia zawadi hii ya ajabu. Katika sherehe ya Noeli tunamshangilia mtoto huyu aliyezaliwa, mtoto aliyezaliwa kutokana na muunganiko wa yale ya mbingu na ya duniani Yesu Kristo Bwana wetu. Katika mashangilio tunaofanya ziko hotuba kutoka kwa malaika, kutoka kwa wachungaji. Ziko nyimbo kutoka kwa malaika, lakini wapo pia wageni ambao hawajakaribishwa yaani mamajusi. Hawa wanaleleta zawadi kwa mtoto aliyezaliwa. Yupo pia mgeni mwingine ambaye hajakaribishwa. Huyu ni Herode ambaye anataka kuyatoa maisha ya mtoto. Leo katika sherehe za Noeli tunaalikwa kusherehekea ndoa, ambayo imekuwa sherehe ya mtoto aliyezaliwa. Kwa sababu kwa kuzaliwa kwake, viumbe vyote vinazaliwa upya. Kwa ajili yetu mtoto amezaliwa.
Sala Ee Yesu uliyelala katika hori la kulia ng’ombe, unyenyekevu wako wa kuwa mwanadamu, utujaze matumaini katika maisha yetu, tujue kwamba Mungu yupo pamoja nasi na kwamba hatuko peke yetu hata katika mauti. Amina.
@ Claretian Publication