Mtakatifu Bernward Wa Hildesheim, Askofu
20/11/2023```
______________________
Masomo Ya Misa
_1Mak 1:10-15, 41-43,
_54-57, 62-64_
_Zab 119:53, 61, 134,_
_150, 155, 158_
_Zab 147:12, 15_
_Lk 18:35-43_
KUWA NA MSIMAMO MZURI KUNA MANUFAA
Injili ya leo ina simulizi la mtu aliyetaka kusaidiwa. Mtu huyu alikuwa mwombaji kwa sababu ya tatizo lake la upofu. Lakini, pia, aliujua uwezo wa Yesu kwani alikuwa tayari amepata kusikia kumhusu. Watu walijaribu kumzuia asipate msaada kutoka kwa Yesu, lakini yeye alisimama imara na kuendelea kuweka msisitizo. Yesu kwa kujua hilo, aliamua kumtimizia haja yake. Kutoka kwa Yesu, aliomba apate kuona. Hili lilikuwa zaidi ya pesa na vyakula alivyokuwa anwaomba watu. Alifahamu vyema kuwa, mara akipata kuona, ataepukana na kuwa ombaomba kwani atajifanyia kazi. Yesu anamfanya aone. Ni mara ngapi sisi hupata nafasi ya kuomba kitu lakini tunaomba visivyo. Huenda sisi huomba mabaya yawapate wale waliotutendea sivyo. Pengine sisi huomba vitu vya anasa ili tuwaringie wenzetu. Tuwe watu wa kuwaza kindani kabla ya kuomba. Tena kama huyu mwombaji wa siku ya leo, tuwe na msimamo dhabiti tuombapo. Leo hii tunashuhudia watu wakiyumbayumba kiimani, akiingia kwenye dini hii, anatoka na kesho yu kwingine. Tuwe na msimamo tuombapo.
Sala
Bwana utuponye kutokana na vilema vyetu hasa vya kukosa msimamo wa imani.*Amina.*_