Mtakatifu Catherine Laboure, Mtawa
MAMLAKA NI YA MUNGU:
Danieli aliweza kumtafsiria mfalme Nebukadreza namna falme zitakavyoishia na ufalme mwingine wenye nguvu kuchukua nafasi. Yesu naye anawaeleza wale waliokuwa wakilistaajabia hekalu lilivyopambwa ya kuwa, hayo yote yana mwisho. Ni Ufalme wa Yesu tu ambao hautakuwa na mwisho. Anawahamiza watu watulie licha ya yanayotukia, wamtegemee yeye nao watasalimika. Tunapotafakari juu ya mamlaka, tunaona kuwa uongozi umewekwa ili uratibishe mambo yaende inavyotakiwa. Mtaalamu mmoja kwa jina Seneca alisema “Aliye na nguvu nyingi, azitumie kidogo kwa busara.” Kunao viongozi wanaotumia mabavu kutawala. Mwisho, mambo hayaendi vyema na wao huishia kuumbuliwa kama mfalme Nebukadreza. Tusisahau kuwa utawala hutoka kwa Mungu na hivi mtawala hutakiwa awatawale watu wake akijua kuwa Mungu ndiye mkuu. Viongozi wanaalikwa kumwogopa Mungu, wakielewa kuwa Mungu ndiye anayeratibisha yote. Hakuna aliye na mamlaka zaidi yake. Vyote vilivyojengwa na mwanadamu, havina udumifu kama Mungu hajahusishwa. Ndio maana Yesu kasema, “Halitasalia jiwe juu ya jiwe, yote yatabomoshwa.” Tujiulize leo, Je tunamshirikisha Mungu katika maamuzi na mipango yetu?
Sala
Tunawaombea viongozi wote ili Mungu awape neema ya kutawala kwa busara za Kimungu.Amina.
@Clerations Publication