MTOTO NI FURAHA KWA FAMILIA NA KWA JAMII
Wakristo Wakatoliki (mume na mke) wanapofunga ndoa, katika maswali msingi wanayoulizwa kabla ya kuweka kiapo chao ni, “Je mko tayari kuwapokea kwa mapendo watoto mtakaopewa na Mungu na kuwalea kama ilivyo sheria ya Kristo na Kanisa lake?” Watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu. Ndio maana Elizabeti anapojifungua, watu wote wanafurahi naye. Babaye anauanza ulezi wake kwa kumpa jina sahihi. Wapo wazazi wanaowapa watoto wao majina yasiyofaa. Majina haya hata huleta madhara katika maisha yao. Majina mengine hata huwa ni chanzo cha ugomvi kati ya wazazi. Mbona mzazi atamke maneno kama ‘Sikutegemea, wewe ni Shida, au hata Sikudhani’ tunapozungumza kuhusu majina ya kuwapa watoto? Leo tujifunze kuwapa watoto wetu majina mazuri, na yenye faraja kama vile Paulo, Petero, Simoni, Karoli, Magdalena. Haya ni majina ya Watakatifu. Wazazi wanahimizwa washirikiane katika malezi. Mtoto asilee na mzazi mmoja mwingine akiwa anajistarehesha. Hili ni janga na ni dhambi. Hivi vituo vya kuwalea watoto ni ishara ya jamii iliyopotoka na wazazi wasiowajibika.
Sala Baba Mwenyezi, tunaomba uwajalie wazazi neema ya kujitambua na kuwapa watoto wao majina yenye utakatifu.Amina.
@Claretion Publication