Juma La 34 La Mwaka
Mtakatifu Bibiana,Bikira Na Shahidi
Masomo Ya Misa
Dan 7:15-27
Dan 3:82-87
Yak 1:18
Lk 21:34-36
ANASA ZA DUNIA NI KIKWAZO KWA WOKOVU
Utawala wowote hapa duniani, kama hautajikita katika kuamini uwepo wa Mungu, hautadumu. Baba wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, pamoja na kazi zake nyingi za kiserikali, kamwe hakuacha kusali na kutoa fursa kwa wengine kuwa na uhuru wa kuabudu, aliishia kusema, “Serikali haina dini.” Na aliyaishi aliyoyasema akimpa Mungu nafasi ya mwanzo. Si ajabu kuwa juhudi zinaendelea za kutawazwa kwake kuwa Mwenye Heri. Katika somo la kwanza, Danieli anaonyeshwa jinsi ambavyo mamlaka ya ulimwengu huu yanavyoishia. Wako watu wakipata mamlaka wanamsahau Mungu. Somo hili linatukumbusha kuwa mtawala wa yote ni Mungu. Hii inapelekea wengine kutumbukia kusiko kama Injili inavyosema, “Ulafi, ulevi na mahangaiko ya maisha.” Luka, katika kusema hivi anaonyesha kuwa, haya yote ni ya mpito. Kristo anatuasa tukeshe tukiomba na lengo liwe ni kufikia wokovu.
Sala
Bwana Yesu Kiongozi mwema, tunaomba uwajalie viongozi wetu Hekima ya kutawala kwa haki. Amina
@ Claretian Publication