UTUKUFU WA MUNGU UKO NASI
Kuzaliwa kwa Kristo kati yetu kumeondoa giza na kuleta nuru ya matumaini na hivi tunaalikwa sote tuwe na mapendo safi na kukaa katika nuru hii kama Yohane anavyotuasa katika somo la kwanza. Nuru hii ndiyo inayotusaidia tumtambue na kumpokea Kristo kama Simeoni alivyompokea kule Hekaluni Yerusalemu. Roho Mtakatifu ndiye mwezeshaji wa yote haya. Tujiulize, Je, tunapompokea Yesu wa Ekaristi, tunakuwa na hali na utayari kama alivyokuwa Simeoni? Huyu mzee alikuwa na shauku kubwa hivyo kwamba alipopata bahati ya kumpokea Yesu mkononi alitamani hata kifo. Alifikia hatua hii kwa vile alikuwa safi kiroho na hakutaka tena utukufu huu aliouona na kuupokea uje uchafuliwe tena na dhambi. Tunapompokea Yesu wa Ekaristi tunashauriwa kuwa safi daima na pia tujue ni tendo la shukrani kwa Mungu kupenda kuwa nasi katika Ekaristi ili kuendelea kutuhuisha kila mara.
Sala
Ee Yesu wa Ekaristi, utupe daima neema na mastahili ya kukupokea vyema ipasavyo. Amina.
@ Claretian Publication