USHINDI NI KWA MUNGU DAIMA
Kawaida mwanadamu hufurahia ushindi. Nchi nyingi duniani zina tarehe maalumu ya kufurahia uhuru wao, wakati waliwashinda wakoloni na kujinyakulia madaraka. Tarehe tisa na tarehe kumi na mbili, mwezi wa Desemba, Tanzania na Kenya mtawalia, husherehekea siku zao za uhuru. Kwenye somo la kwanza, Yuda na nduguze wanasherehekea ushindi dhidi ya adui waliowataka waiasi imani yao. Kote ulimwenguni, tarehe 25 Desemba, Wakristo husherehekea Noeli (Mungu Mwana kuzaliwa kati yetu ili aliondoe giza la dhambi). Sisi Wakatoliki pia husherehekea Pasaka (Kristo kufufuka baada ya mateso na kifo-fumbo la ukombozi wetu), Pentekoste (Roho Mtakatifu kulishukia Kanisa). Hizi na sikukuu nyinginezo, zalenga kutuimarisha kiimani. Maadhimisho haya nyakati za mamabu, yalifanyika katika maeneo maalumu yaliyotengwa rasmi. Kristo katika Injili anaonyesha umuhimu wa kuyaheshimu maeneo husika ambayo kwa sasa ni pamoja na makanisa. Tuyaheshimu na kuyatumia makanisa kupata baraka na utulivu tunaouhitaji ili kuwasiliana na Muumba wetu bila makelele na fujo ziwazo kwenye kumbi za burudani, na kwenye viwanja vya michezo.
Sala
Utujalie Ee Bwana tuweze kutoa heshima kwa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya sala. Amina.
@Claretian Publication