MOYO USIO NA SHUKRANI HUYAKAUSHA MEMA YOTE
Wahenga wanasema, “Kushukuru ni kumoba tena” Kuna watu katika maisha yao ambao swala la kushukuru ni msamiati usiojulikana. Hata akitendewa jambo jema kiasi gani, yeye huona ni haki yake na hivyo hana haja ya kushukuru. Katika somo la kwanza, Hana anamshukuru Mungu baada ya kumtendea makuu. Ni wangapi tulio na moyo wa kusema asante au hata kukumbuka kushukuru? Bikira Maria katika Injili anaonyesha moyo wa shukrani na unyenyekevu kwa Mungu. “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana….” Unyenyekevu huu ndio anaokuja kuwa nao Kristo, ni kama anaambukizwa na mama yake. Ndipo tunaambiwa, “Tazama mfalme anakuja……ni mnyenyekevu” (Zek 9:9). Mzazi akiwa na tabia njema, huwa ni rahisi watoto wake kuwa na tabia kama hiyo. Leo tujifunze kuwafunza watoto wetu kuwa na moyo wa shukrani na unyenyekevu.
Sala Ee Bwana, kwa maombezi ya Bikira Maria, tunaomba neema zako ili tuweze kukushukuru kwa mema unayotutendea.Amina
@ Claretian Publication