WATOTO HAWASTAHILI KUUAWA
Herode alikuwa mtu mwovu hata akamuua mkewe na kuuhifadhi mwili wake katika asali. Aliwanyonga wanawe wawili hadi kufa. Mara kwa mara aliwaua wale wote waliokuwa wanaonyesha kukosa uaminifu kwake. Ni Herode huyu ambaye mtoto wake alimkata kichwa Yohane Mbatizaji. Aliwatisha Yosefu na Maria hata wakakimbilia Misri. Ni ukatili na unyama huu wa Herode ndio unaotufanya tufanye kumbukumbu hii ya watoto mashahidi. Herode alitoa tamko la kuwaua watoto wote wa kiume katika Betlehemu na kando kando yake kwa lengo la kumwangamiza mtoto Yesu. Hawa watoto mashahidi ndio mashahidi wa kwanza katika Kanisa. Inaonekana hawa walikufa badala ya Kristo. Historia na Maandiko Matakatifu yanaonyesha kwamba wasio na hatia wanakufa kusudi mmoja aweze kuishi na kukamilisha utume. Wengi kati ya watoto hawa mashahidi, hawakupata nafasi hata ya kucheza michezo ya kitoto. Watoto mashahidi walikuwa ni kama Kristo mwingine. Inawezekana watoto mashahidi wako karibu kabisa na altare ya Mungu huko mbinguni. Watoto hawana hatia, lakini wao wanakufa kifo cha kikatili kabisa kusudi ukombozi ukamilike.
Sala Enyi watoto mashahidi, mlioanguka kwa mikono ya mtu mwovu, kwa damu yenu, muwafae wanaoteseka na kuangamizwa kwa ajili ya haki.Amina.
@ Claretian Publication