MVUVI MKUU ANAKUA MTUME WA YESU
Andrea alikuwa mvuvi kutoka Betsaida, naye aliishi karibu na pwani ya bahari ya Galilaya. Humo Galilaya, mingi kati ya miujiza ya Yesu ilitendeka. Wengi kati ya mitume wa Yesu walikuwa wavuvi ambao, kama wakulima, hutegemea sana kudra za Mwenyezi Mungu katika mafanikio yao. Mvuvi humtegemea Mungu ili samaki wajae wavuni, kama vile mkulima humtegemea Mungu kwa mvua. Wao hufanya bidii ili humtumainia Mungu zaidi. Hizi ndizo sifa alizo nazo Andrea na wavuvi wenzake. Kwanza huyu alikuwa mfuasi wa Yohane Mbatizaji, kisha akamfuata Yesu, wakiwa na nduguye Simoni. Yako mapokeo mbali mbali ambayo yanaeleza kule Andrea aliinjilisha baada ya kupaa mbinguni Bwana wetu Yesu Kristo. Lakini ukweli juu ya kifo chake haujulikani japo mapokeo mengine yanasema alifungwa katika msalaba, na akawa akihubiri hapo juu kwa siku kadhaa hadi mauti yalipomkuta. Andrea na mitume wenzake walikuwa watu wa kawaida ila walikuwa wenye imani. Waliimarishwa na Kristo na kuyatenda makuu. Tuwaige mitume katika kumwamini Mungu. Yesu atatuimarisha nasi tutayatenda makuu hata na zaidi.
Sala Ewe Mtakatifu Andrea, kwa maombezi yako, wasaidie Wakristo wote wawe wakarimu katika kuitikia mwito wa Bwana na kumfuata.Amina.
@ Claretian Publication