KUHESHIMU WAKUBWA NI FADHILA
Kanisa leo linaadhimisha sikukuu ya Yohane Mwinjili. Huyu ni kati ya mitume waliokuwa karibu sana na Yesu na hivi waliona mengi. Katika maisha yake tunaona fadhila ya unyenyekevu na utii kwa wakubwa. Injili imetueleza kuwa, habari za ufufuko wa Yesu zilipowafikia, walifunga safari kwenda kaburini. Japo yeye Yohane alikuwa wa kwanza kufika kaburini, hakuingia hadi Petro alipofika na kuingia kwanza. Hii ni ishara ya heshima. Sehemu nyingi leo hii mambo hayaendi sawa kwa vile kila mtu anajifanya kuwa mjuaji. Heshima na utii havimo tena kwenye msamiati wetu tulioendelea. Twaweza kuwa watendaji wazuri lakini tunaharibu pale tunapokosa heshima. Mwinjili Yohane ameandika mengi na yanadumu kutokana na tabia yake ya kuheshimu wakubwa. Alisisitiza sana juu ya ‘kupendana kindugu’. Leo hii tunaalikwa kweli kupendana daima.
Sala
Mungu Mwenyezi, kwa maombezi ya Mtakatifu Yohane Mwinjili, tujalie kuwa na fadhila ya kuwaheshimu wakubwa wetu. Amina.
@ Claretian Publication