MALEZI MAZURI HUKOLEZWA NA SALA
Wazazi wa Yesu (Mt. Yosefu na Bikira Maria) walifuata sheria na desturi za ile jamii na walizingatia pia taratibu za malezi kuwa na mtoto wakati wote katika hatua zake zote za kukua. Vijana wengi leo hii wana tabia potovu, kutokana na kutokuwa na wazazi wao. Tunamwona Yesu akirudi na wazazi wake na anaendelea kukua katika hekima na neema za Mungu. Hii ni dalili ya wazi kuwa, kwa hekima hiyo, alikuwa anawatii na kuwaheshimu wazazi wake. Vijana siku hizi hawana heshima kwa wazazi wao. Unamkuta kijana akijibizana na hata kumtukana mzaziwe. Hata wazazi wengine hawathubutu kuwaonya watoto wao. Hata pale mtoto haishi visivyo, utamwona mzazi hamsuti, ameiasi kazi yake ya kulea. Hii inachangiwa pia na wazazi kukosa moyo wa sala kama ule wa Ana (binti Fanueli), anayekesha akisali. Kwenye dunia ya leo, ukionekana unasali, utasemwa kuwa wewe u mnafiki, au hata usemekane unajipendekeza kwa viongozi wa Kanisa. Hali hii inawafanya wengi kuogopa kuwa na moyo wa sala.
Sala Mama Bikira Maria tuombee neema ya kuyatoa malezi bora kwa watoto wetu hasa vijana wetu na uwajalie moyo wa usikivu.Amina.
@ Claretian Publication