FAMILIA NJEMA NI CHIMBUKO LA KANISA
Masomo ya leo yanazungumzia juu ya familia. Kwenye somo la kwanza tunawaona Manoa na mkewe na kwenye Injili Zakaria na mkewe Elizabeti. Familia zilikuwa zinamcha Mungu lakini hazikuwa zimejaliwa baraka ya mtoto/watoto. Mungu kwa mpango wake anamtuma malaika kwao kuwapa baraka ya mtoto. Tunajifunza kuwa, hakuna mtoto azaliwaye bila mpango wa Mungu. Pia Mungu anao mpango kwa kila familia. Kwenye ulimwengu wa leo, tunashuhudia magomvi kati ya wanafamilia. Wengine wanatengana eti kwa vile mmoja wao hana uwezo wa kuzaa au kuzalisha. Au hata wengine kwa vile mke anapata tu watoto wa kike. Wao hukosa kuelewa kuwa mpango wa mtoto ni wake Mungu. Wengine hutafuta imani za kishirikina au kuhamia kwenye dini nyingine ili kutafuta miujiza au hata kukwepa taratibu za mke mmoja. Msidanganyike. Tusiingie kwenye mitego ya watu wanaojitafutia kipato. Mungu pekee ndiye mwenye uwezo wa kuyawezesha yote.
Sala Tunakuomba Baba Mwenyezi uzijalie familia zetu neema ya kutulia hasa inapotokea gumu kimaisha. Amina.
@ Claretian Publication