TAFAKARI YA JUMATATU
HATUWEZI KAMWE KUUKWEPA MPANGO WA MUNGU
Kanisa Takatifu Katoliki linaheshimu na kutunza Sakramenti Saba tulizoachiwa Kristo. Mojawapo ni Sakramenti Takatifu ya ndoa. Hii ni kati ya mume na mke ambao kabla ya ndoa huwa na kipindi cha uchumba. Hiki ni kipindi kitakatifu na wahusika wanapaswa kukitumia vyema kwa ajili ya maisha yao ya baadaye. Vijana wengi leo hii wanatumia visivyo kipindi hiki. Wengi hukitumia kama kipindi cha kufanya uhuni, kujaribu eti kama mwenzake anaweza kuzaa au la! Hiku ni kuuweka mpango wa Mungu pembeni. Mt. Yosefu akiwa na Bikira Maria alikipitia kipindi cha uchumba. Ila wakati huo akaona mabadiliko kwa mwenziwe na hivyo akaamua kumwacha kwa siri. Mungu aliingilia kati na kuwa huo ulikuwa mpango wake. Papo hapo Mt. Yosefu akayatii mapenzi ya Mungu. Tujifunze kutoka kwa Mt. Yosefu, kutopenda kuwaaibisha wenzetu hata pale ambapo wamefanya visivyo. Tuweni na utu, tuwe watu wa sala na kuomba uelewano kati yetu. Tuuheshima uchumba na tuziheshimu ndoa.
Sala Ee Mt. Yosefu, tuombee neema ya kupokeana vyema katika maisha yetu hasa kwa vijana wanaojiandaa kwa maisha ya ndoa.Amina.
@ Claretian Publication