DAIMA MUNGU HUFURAHIA TOBA
Baada ya wazazi wetu wa kwanza kumuasi Mungu na kuanguka katika dhambi, Mungu kwa mpango wake bado aliendelea kuonyesha Huruma yake kwa mwanadamu. Alikazania kumpenda manadamu aliyemuumba kipekee tofauti na viumbe wengine kwani kabeba sura na mfano wake. Kamwe hangetaka mwanadamu apotee. Kwenye somo la kwanza, nabii Isaya anajaribu kuchambua kwa kina hali itakavyokuwa. Anamwalika mwanadamu kutega sikio na kuitikia mwaliko huu wa Mungu kumtaka amsikie yeye, alisikie na kulitii neno lake. Anamhimiza mwanadamu kukubali kukumbatiwa na Mungu kifuani mwake kama kondoo (unyenyekevu). Mwinjili Matayo naye anatuonyesha furaha anayokuwa nayo Mungu, pale ambapo mdhambi anatubu. Mfano wa kondoo aliyepotea unatuhusu sote. Ni kwa namna gani tunatilia maanani Sakramenti ya Kitubio ili asipotee hata mmoja? Je sisi huenda maungamo kwa sababu tu wale wengine wanaenda? Tunaalikwa kuwa kama huyu kondoo mmoja, aliyetafutwa na mchungaji, naye akakubali kupatikana na kubebwa akirejeshwa kwenye zizi. Unao umuhimu kwake Mchungaji Mwema. Jambo hili likujenge kiimani umruhusu Mchungaji akubebe mabegani mwake ili afurahi, nawe utaurithi Uzima wa Milele. Msikilize Yeye na uyatende akuahizayo.
Sala
Ee Yesu tunaomba utujalie neema ya kuthamini na kuitumia vyema Sakaramenti ya Kitubio. Amina.
@ Claretian Publication