“LITAWEZEKANAJE NENO HILI..?”
Hekima ya hali ya juu ya mwanadamu ni kutambua kwamba Mungu alimtuma Mwanawe ulimwenguni kuivunja minyororo ya dhambi. Furaha kubwa kabisa ya wanadamu, ni kuwa na amani ya Kristo. Baraka kubwa ya wanadamu ni kuwa na matumaini kwamba baada ya kifo, wafuasi wa Kristo watatawala pamoja naye. Mungu aliweka katika Maria upendeleo wa pekee kwa njia ya neema zake, ili kwa vyovyote vile Maria aongozwe kwa neema zake. Maria alisadiki. Imani yake ilikuwa na unyenyekevu kiasi kwamba alianza kusadiki aliyoambiwa na malaika ndipo akaanza kujiuliza. Swali la Maria kwa malaika lilikuwa sahihi kabisa, “Litawezekanaje neno hili..?” Malaika alikuwa akizungumzia jambo ambalo kwa wanadamu haliwezekani. Umebarikiwa na Bwana. Utapata mtoto. Maria alijijua mwenyewe kuwa bikira ila alisadiki. Na kilichofuata kilikuwa kinaumiza kichwa zaidi, atakuwa mkuu ataitwa Mwana wa Aliye juu. Hapo ndipo Maria alipopata kuuliza swali lake, “Litawezekanaje neno hili?” Hilo laweza kuwa swali letu sote; Litawezekanaje hili? Tutawezaje kutoka katika janga hili la Korona? Tunawezaje kupata suluhisho la matatizo yetu? Inawezekanaje tuwe na amani katika ulimwengu uliojaa magaidi? Je! tunakumbuka maneno ya malaika kwamba atakuwa Mkuu ataitwa Mwana wa Aliye juu, naye atamiliki nyumba ya Yakobo milele. Hili linatuonyesha kwamba kwa Mungu yote yanawezekana. Katika ulimwemgu huu wa wanadamu dhaifu, huwa tunashawishika kuuliza swali kama alilouliza Maria, “Litawezekanaje neno hili?” Ni jambo gumu kupata majibu ya maswali kama haya. Ndipo tunatakiwa tuisome Injili kwa uangalifu, “Hakuna lisilowezekana kwa Mungu.”
Ndio ninayaogopa magonjwa, ninaogopa kuzeeka, ninaogopa majanga mbali mbali yajayo, ninaogopa kuwa siku za usoni maji safi huenda yasipatikane, kwa sababu ya uharibifu wa mazingira. Bwana linawezekanaje neno hili? Leo ni Dominika ya nne ya Majilio. Ninaungana na Bikira Maria aliyesema, “Litawezekanaje neno hili?” Lakini nikiongozwa na imani, mwisho nitasema, Mimi ni mjakazi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema.” Yako mambo manne ambayo tunapaswa kuyafanya: kwanza tuulize swali, pili tusikilize, tatu tuwe na imani, nne tukumbuke kwamba Mungu alikuja na kukaa ndani yetu. Masia aliyetabiriwa na nabii Nathani katika kitabu cha Samweli alikuja katika nafsi ya Yesu. Sasa anakuja kwa kila mmoja wetu kwenye sherehe za Noeli. Japokuwa sisi ni wadhambi, Kristo anatualika siku yake ya kuzaliwa, kwa sababu hakuna lisilowezekana kwa Mungu.
Sala Ee Bwana Yesu, tunaomba kama Maria Mama yako, tulitii Neno la Mungu, ili nasi tumbebe Kristo katika roho zetu na kumpeleka duniani kote. Amina.
@ Claretian Publication