MASOMO YA MISA
Isa. 63:16-17; 64:1, 4-8
Zab. 80:1-2, 14-15, 17-18 (K) 3
1 Kor. 1:3-9
Zab. 85:7
Mk. 13:33-37
SISI SOTE TUMEKUWA KAMA MTU ALIYE MCHAFU
Kipindi cha Majilio kinatualika kumngojea Bwana. Nabii Isaya anaonyesha tamaa yetu kubwa tunapomngoja Bwana, “Pasua mawingu ushuke” (Isa 64:1). Mt. Paulo naye anawahakikishia Wakorintho kwamba hawatapungukiwa zawadi za kiroho wanapongoja kufunuliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Katika somo letu la Injili, Yesu anatukumbusha kukesha. Kwa hakika tunapaswa kumngoja Bwana atakayekuja saa ya kufa kwetu. Kifo hakimheshimu mtu yeyote, bali kinaweka mkono wake hata kwa mfalme. Majilio ni kipindi ambacho kinatualika kuwa tayari wakati wote tukimngoja Bwana. Lakini sisi kama Wakristo hatupaswi kujiweka tayari kwa siku ya mwisho Kristo atakapokuja tu, bali tunapaswa kujiweka tayari kwa ujio wake kila siku ya maisha yetu. Kama tukiwa makini tutamwona Yesu akitokea katika maisha yetu ya kila siku. Tufanyeje ili tuwe tayari? Isaya ansema kuwa sote tumekuwa wachafu, na wenye unajisi, tumenyauka kama jani, na kuchukuliwa na upepo. Anatualika tuyajenge maisha yetu katika ukweli huu kwamba sisi ni wakosefu, sisi ni wadhambi. Ukweli unapswa kutukumbusha kuwa hatustahili mbele za Bwana. Ila tujiachilie kwake tukisema, “Wewe uchungaye Israel Usikie, wewe uketie juu ya makerubi utoe nuru uziamshe nguvu zako uje utuokoe.” Hili ndilo tunapaswa kufanya katika kipindi cha Majilio. Tuwe na matumaini tukiangalia mbele, bali pia tuangalie nyuma na kukubali kwamba tumekwenda mbali sana kutoka katika njia ya haki. Katika Majilio tunalia tukisema, “Njoo, njoo Immanuel tunakuhitaji.” Tunapowakaribisha wageni nyumbani kwetu, sisi hujiandaa vilivyo. Mgeni tunayemtarajia ni mgeni wa thamani na mashuhuri. Huko ndiko kukesha. Tumaanishe tunachokisema tusemapo Njoo. Tujiandae kwa kusawazisha njia na kuondoa vikwazo ambavyo vinatuzuia kumpokea Mwokozi wetu. Je ni dhambi? Ni vitabia visivyoendana na anayoyaamuru Mungu? Tumwalike Mungu aziamshe nguvu zake aje atuokoe.
Sala Ikiwa tuna macho ya kuona na masikio ya kusikia, utujalie Ee Bwana, Noeli iwe ni kiashiria kinachotuonyesha ujio wa Kristo kila siku ya maisha yetu. Amina
@ Claretian Publication