RANGI YA KILITURJIA: NYEKUNDU ♥
SOMO LA KWANZA
2 WAKORINTHO 9:6b—10
Mungu anampenda anayetoa kwa furaha.
Somo katika barua ya pili ya Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho
Ndugu: Anayepanda haba, atavuna haba; anayepanda vingi atavuna vingi. Kila mtu atoe kama alivyonuia moyoni mwake, si kwa huzuni wala kwa shuruti, kwa maana Mungu anampenda anayetoa kwa furaha. Mugnu ana uwezo wa kuwamwagia riziki ya kutosheleza mahitaji yenu yote ya kila wakati na hata kuwabakizieni kitu kutenda mema mengine, kama ilivyoandikwa: “Anagawa na kuwapa fukara. Uadilifu wake wadumu milele.” Mungu anayempa mpanzi mbegu kwa kupanda na mkate kwa kula, atawapa ninyi pia mbegu kwa kupanda na mkate kwa kula, atawapa ninyi pia mbegu na kuiotesha, na atasitawisha mazao ya uadilifu wenu.
NENO LA BWANA… TUMSHUKURU MUNGU
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 112:1b—2, 5—6, 7—8, 9 (K. 5a)
K. Heri mtu mwenye kukopesha kwa ukarimu.
Heri mtu yule amchaye Bwana,
anayependezwa sana na amri zake.
Wazao wake watakuwa wenye nguvu katika nchi,
kizazi cha wenye adili kitabarikiwa. K.
Heri mtu mwenye kukopesha kwa ukarimu,
mwenye kuyafanya mambo yake kwa haki.
Maana hatatikisika kamwe;
wenye haki watakumbukwa milele. K.
Hataogopa habari mbaya;
moyo wake u thabiti, ukimtumainia Bwana.
Moyo wake ni mtulivu, hana woga,
mpaka awaone adui zake wameshindwa. K.
Kwa ukarimu huwasaidia maskini;
uadilifu wake utadumu milele;
nguvu yake itainuliwa juu kwa utukufu. K.
SHANGILIO LA INJILI
YOHANE 8: 12bc
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana; anifuataye mimi atakuwa na nuru ya uzima.
W. Aleluya.
INJILI
YOHANE 12:24—26
Mtu akinitumikia, Baba yangu atamheshimu.
† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Yohane
Wakati ule: Yesu aliwaambia wafuasi wake, "Amin, amin, nawaambieni, chembe ya ngano isipoanguka ardhini na kufa, inakaa hali hiyo hiyo peke yake; lakini ikifa, inatoa mazao mengi. Yeye aipendaye nafsi yake ataipoteza, na aichukiaye nafsi yake ulimwenguni hapa ataiokoa kwa uzima wa milele. Mtu akitaka kunitumikia, anifuate; na nilipo mimi, mtumishi wangu atakuwapo pia. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu."
INJILI YA BWANA... SIFA KWAKO EE KRISTO