RANGI YA KILITURJIA: NYEUPE 🤍
SOMO LA KWANZA
DANIELI 7:9—10, 13—14
Vazi lake lilikuwa jeupe kama theluji.
Somo katika kitabu cha Nabii Danieli
Nilikuwa nikiangalia, [katika maono yangu]: Viti vya enzi vikawekwa, na Mzee wa Kale akaketi. Vazi lake lilikuwa jeupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; kiti chake cha enzi kilikuwa ndimi za moto, na magurudumu yake moto wenye kuwaka. Mto wa moto ulitiririka na kutoka mbele yake; maelfu na maelfu walimtumikia, na milioni na milioni walisimama wima mbele yake. Wenye kuhukumu barazani wakaketi, vitabu vikafunguliwa. Nikaangalia katika maono yangu ya usiku, na tazama, mmoja kama mwana wa mtu akaja katika mawingu ya mbingu, akaendelea mpaka akamfikia yule Mzee wa Kale, akakaribishwa mbele yake. Akapewa utawala, utukufu na ufalme: watu wa makabila yote na mataifa yote na lugha zote wakamtumikia. Utawala wake ulikuwa utawala wa milele usiopita, na ufalme hautaangamizwa.
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 97:1—2, 5—6, 9 (K. tazama 1a, 9a)
K. Bwana ametamalaki, Aliye Juu, juu sana kuliko nchi yote.
Bwana ametamalaki; nchi na ishangilie;
visiwa vingi na vifurahi.
Mawingu na giza vyamzunguka Bwana;
hukumu na haki ni msingi wa kiti chake. K.
Milima imeyeyuka kama nchi, mbele ya uso wa Bwana,
mbele za Bwana wa dunia yote.
Mbingu zinatangaza haki ya Mungu;
na mataifa yote wameuona utukufu wake. K.
Maana wewe ndiwe Bwana, Uliye Juu,
juu sana kuliko nchi yote,
umetukuka sana juu ya miungu yote. K.
SOMO LA PILI
2 PETRO 1:16—19
Sauti hiyo iliyotoka mbinguni tuliisikia.
Some katika barua ya pili ya Mtakatifu Petro
Wapendwa: Hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu tulipowahubiria enzi ya Bwana wetu Yesu Kristo na kufika kwake, bali tulikuwa mashahidi wenyewe tulioona kwa macho yetu utukufu wake. Maana aliheshimiwa na kutukuzwa na Mungu Baba na utukufu mkuu alipofikiwa na sauti na kuambiwa: "Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye." Sauti hiyo iliyotoka mbinguni tuliisikia tulipokuwako pamoja naye juu ya mlima mtakatifu. Hivyo tumethibitishwa neno la manabii. Nanyi mnafanya vyema kuutumia unabii kama taa iangazayo gizani mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu.
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
SHANGILIO LA INJILI
MATHAYO 17:5c
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Huyu ni mwanangu mpendwa, anipendezaye; msikilizeni yeye.
W. Aleluya.
INJILI
MATHAYO 17:1—9
Uso wake uling'aa kama jua.
† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo
Wakati ule: Yesu aliwachukua Petro na Yakobo na ndugu yake Yohane, akawapeleka hao peke yao juu ya mlima mrefu. Akageuka sura mbele yao. Uso wake uling'aa kama jua. Mavazi yake yakawa meupe kama mwanga. Mara Musa na Eliya wakawatokea na kuzungumza naye. Petro akaanza kusema, akamwambia Yesu, "Bwana, yatufaa kukaa hapa. Ukipenda, tujenge hapa vibanda vitatu, kimoja chako, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya." Wakati anasema maneno hayo, tazama, wingu angavu likawatandia. Mara sauti ikatoka katika wingu lile ikisema, "Huyu ni Mwanangu mpendwa, anipendezaye; msikilizeni yeye." Wafuasi waliposikia hayo, walianguka kifudifudi, wakaogopa sana. Yesu akajongea, akawagusa, akasema, "Simameni na msiogope." Wakainua macho yao wasione mtu isipokuwa Yesu peke yake. Waliposhuka kutoka mlimani, Yesu aliwaonya, "Msimwambie mtu habari ya maono haya mpaka Mwana wa Mtu atakapokuwa amefufuka katika wafu."
INJILI YA BWANA... SIFA KWAKO EE KRISTO