SOMO 1
Warumi 10:9—18
Ndugu: Ukiungama kwa kinywa chako, Yesu ni Bwana, na ukisadiki moyoni mwako Mungu amemfufua katika wafu, utaokoka. Kwa moyo mtu husadiki apate uadilifu, kwa kinywa huungama imani, apate wokovu. Kwa maana Maaandiko yasema: "Kila amsadikiye hataaibishwa." Ndiyo maana hakuna tofauti baina ya Myahudi na Mgiriki. Bwana wa wote ni mmoja huyu huyu, ni mkarimu kwa wote wamwitao. Maana kila anayeliita jina la Bwana ataokoka. Lakini watamwitaje wasiyemsadiki? Au watamsadikije wasiyesikia habari zake? Au watasikiaje pasipo mhubiri? Au watu watahubirije wasipotumwa? Kama ilivyoandikwa, "Ni mizuri kama nini miguu ya wenye kutangaza habari njema ya majaliwa mema!" Lakini sio wote waliitii habari njema, kwa maana Isaya asema, "Bwana, ni nani aliyesadiki mahubiri yetu?" Basi, imani hupatikana kwa njia ya mahubiri, na mahubiri chemchemi yake ni neno la Kristo. Lakini nauliza, je, hawakuwasikia? Sivyo! Wamewasikia: "Uvumi wao umeenea duniani kote, na maneno yao yanasikika hata mipaka ya dunia."
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 19:2—3, 4—5a (K. 5a)
K. Sauti yao yaenea duniani kote.
Mbingu zinaueneza utukufu wa Mungu,
anga linaitangaza kazi ya mikono yake.
Mchana huupasha mchana habari hiyo;
nao usiku huujulisha usiku. K.
Hakuna neno, hakuna usemi;
wala sauti yake haisikiki;
lakini uvumi wake waenea duniani kote,
na maneno yake hata mipaka ya ulimwengu. K.
SHANGILIO LA INJILI
MATHAYO 4:19
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Njooni mnifuate, asema Bwana, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.
W. Aleluya.
INJILI
Mathayo 4:18—22
Wakati ule: Yesu alitembea kando ya Bahari ya Galilaya, akawaona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na nduguye Andrea, wakitupa wavu baharini, kwa maana walikuwa wavuvi. Akawaambia, "Njooni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu." Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Akaendelea mbele, akawaona ndugu wawili wengine, ndio Yakobo, mwana wa Zebedayo, na nduguye Yohane, wakitengeneza nyavu zao chomboni, pamoja na baba yao Zebedayo. Akawaita, mara wakakiacha chombo na baba yao, wakamfuata.
Injili ya Bwana.