SOMO 1
Danieli 5:1—6, 13—14, 16—17, 23—28
Siku zile: Mfalme Belshaza aliwafanyia wakuu wake elfu karamu kubwa, akanywa divai nao. Alipokuwa amelewa kwa ile divai, Belshaza akaamuru viletwe vile vyombo vya dhahabu na fedha, vilivyotolewa na Nebukadneza baba yake, katika hekalu la Yerusalemu, na wakuu wake na wake zake na masuria wake wapate kunywa katika vyombo hivyo. Basi wakaleta vyombo vile vya dhahabu vilivyotolewa katika hekalu la Nyumba ya Mungu huko Yerusalemu, nao mfalme na wakuu wake na wake zake na masuria wake wakanywa katika vyombo hivyo, wakanywa divai wakaisifu miungu ya dhahabu na fedha, shaba nyekundu na chuma, miti na mawe. Saa hiyo hiyo, vikatokea vidole vya mkono wa mwanadamu, vikaandika katika chokaa ya ukuta wa nyumba ya mfalme, mbele ya kinara. Mfalme akaona sehemu hiyo ya mkono wenye kuandika, na hapo mfalme akabadilika rangi usoni; mawazo yake yakamwogopesha, viungo vya kiuno chake vikalegea, na magoti yake yakagongana. Hapo wakamleta Danieli mbele ya mfalme. Naye mfalme akamwuliza Danieli, "Je, wewe ni Danieli, mmoja wa wale waliohamishwa kutoka Yuda na kuletwa huku na baba yangu mfalme? Nimesikia habari zako, ya kwamba roho ya miungu ipo ndani yako, nawe umepatikana kuwa na mwangaza na ufahamu na hekima bora ya ajabu. Nimeambiwa ya kuwa waweza kuagua na kufungua mafumbo. Sasa, ukiweza kusoma andiko hili, na kunijulisha maelezo yake, utavikwa nguo za zambarau, utavaa shingoni mkufu wa dhahabu, nawe utakuwa mtu wa tatu kwenye kutawala ufalme wangu." Hapo Danieli akamjibu mfalme, "Vipaji vyako vibaki kwako, uwape wengine zawadi zako; lakini nitamsomea mfalme andiko hilo na kumjulisha maelezo yake. Ulijikuza juu ya Bwana wa mbinguni, uliagiza wakuletee vyombo vya nyumba yake, nawe pamoja na wakuu na wake zako na masuria wako mkavinywea divai na kuisifu miungu ya dhahabu na ya fedha, ya shaba nyekundu na ya chuma, ya miti na ya mawe, isiyoona wala kusikia wala kufahamu; wala hukumsifu Mungu anayetunza pumzi yako mikononi mwake na kuongoza njia zako zote. Ndiyo sababu ametuma kitanga cha mkono ule, kilichoandika peke yake maandiko yake. "Maandiko yaliyoandikwa ni: MENE, TEKEL, PERES. Maana ya maneno ndiyo hii: MENE: yaani Mungu ameuhesabu ufalme wako na kuumaliza; TEKEL: ndiyo kusema umepimwa katika mizani ukaonekana umekosa uzito. PERES: ufalme wako umegawanywa, nao watu wa Media na Waajemi wamepewa."
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
DANIELI 3:40, 41, 42 43, 44, 45 (K. 40b)
K. Msifuni na kumtukuza milele.
Enyi jua na mwezi, mtukuzeni Bwana,
msifuni na kumtukuza milele. K.
Enyi nyota za mbinguni, mtukuzeni Bwana,
msifuni na kumtukuza milele. K.
Enyi nyote, mvua na manyunyu, mtukuzeni Bwana,
msifuni na kumtukuza milele. K.
Enyi nyote pepo, mtukuzeni Bwana,
msifuni na kumtukuza milele. K.
Enyi moto na joto, mtukuzeni Bwana,
msifuni na kumtukuza milele. K.
Enyi masika na kiangazi, mtukuzeni Bwana,
msifuni na kumtukuza milele. K.
Enyi umande na sakitu, mtukuzeni Bwana,
msifuni na kumtukuza milele. K.
SHANGILIO LA INJILI
UFUNUO 2:10c
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Uwe mwaminifu hata kufa, asema Bwana, nami nitakupa taji la uzima.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 21:12—19
Wakati ule: Yesu aliwaambia wafuasi wake, "Watawakamata ninyi na kuwadhulumu, watawapeleka katika masinagogi na kuwatia gerezani, na mtapelekwa mbele ya wafalme na magavana kwa ajili ya jina langu. Hivyo mtapata nafasi ya kushuhudia. Basi, jikazeni mioyo yenu: msifikirie kabla yake namna ya kujitetea. Kwa maana mimi nitawapa kauli na hekima, hata adui zenu wote watashindwa kupinga na kukaidi. Lakini mtatolewa na wazazi na ndugu na jamaa na marafiki, nao watawaua baadhi yenu. Na mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu. Lakini hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea. Kwa uvumilivu wenu mtaokoa nafsi yenu."
Injili ya Bwana.