SOMO 1
Danieli 2:31—45
Siku zile: Danieli alimwambia mfalme Nebukadneza, "Umeona njozi, ee mfalme, ndiyo hii: sanamu, sanamu kubwa, yenye kung'aa sana, ilisimama mbele yako; umbo lake lilikuwa lenye kutisha. Sanamu hiyo, kichwa chake ni dhahabu safi, kifua na mikono yake ni fedha, tumbo lake na mapaja yake ni shaba nyekundu, miguu yake ni chuma, vidole vyake ni nusu chuma, nusu udongo. Ulipokuwa unaangalia ghafla jiwe likaanguka pasipo kusukumwa na mkono, likaigonga sanamu penye nyayo zake za chuma na udongo, likazivunjavunja. Ndipo zikavunjika pamoja chuma na udongo, shaba nyekundu, fedha na dhahabu, zikawa sawa na makapi kiwanjani wakati wa hari, na upepo ukazipeperusha hata pasionekane kitu. Nalo jiwe lililoigonga sanamu likageuka kuwa mlima mkubwa ulioijaza dunia nzima. Ndoto ndio hiyo: maaguzi yake tutamwagulia mfalme. Wewe, ee mfalme, ni mfalme wa wafalme; naye Mungu wa mbinguni amekupa ufalme na uwezo na nguvu na utukufu; ameweka mikononi mwako wanadamu na wanyama wa pori na ndege wa angani, amekupa kuwatawala hao wote; wewe ni kile kichwa cha dhahabu. Nyuma yako ufalme mwingine utainuka, ulio mdogo kuliko ufalme wako, baadaye utakuja ufalme wa tatu, utakaokuwa wa shaba nyekundu na wenye kuitawala dunia yote. Ufalme wa nne utakuwa na nguvu kama chuma; sawa na chuma chenye kuponda na kama chuma chenye kusaga, ule ufalme utaponda na kusaga falme zote. Uliona miguu na vidole vyake, vilivyokuwa nusu udongo wa mfinyanzi nusu ya chuma, ni mfano wa ufalme uliogawanyika, ila ufalme huo utakuwa na nguvu ya chuma. Kama vile ulivyoona chuma chenye kuchanganyika na udongo wa mfinyanzi, vidole vya miguu vilikuwa nusu chuma na nusu vya udongo, maana yake nusu ya ule ufalme utakuwa na nguvu na nusu utakuwa dhaifu. Nawe uliona chuma chenye kuchanganyika na udongo wa mfinyanzi, maana yake falme hizo zitajichanganya kwa maagano ya ndoa, lakini hazitaungana, kama vile chuma kisivyounganika na udongo. Basi, wakati wa wafalme hao, Mungu wa mbinguni atasimamisha ufalme usioharibika milele, na ufalme huu hautaachwa kwa taifa jingine; utaziponda na kuangamiza falme hizo zote, nao utakaa hata milele. Sawa kama ulivyoona jiwe lenye kukatwa kutoka mlimani, bila kuguswa na mkono, na lenye kuvunja chuma, shaba nyekundu, udongo, fedha na dhahabu. Mungu mkuu amemfunulia mfalme yajayo; ndoto ni hii hasa, na maelezo yake ni ya hakika."
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
DANIELI 3:35, 37, 36, 38, 39 (K. 35b) [au: NV 3:57, 58, 59, 60, 61 (K. 59b)]
K. Msifuni na kumtukuza milele.
Enyi nyote, malaika wa Bwana, mtukuzeni Bwana,
msifuni na kumtukuza milele. K.
Enyi mbingu za Bwana, mtukuzeni Bwana,
msifuni na kumtukuza milele. K.
Enyi maji ya juu ya anga, mtukuzeni Bwana,
msifuni na kumtukuza milele. K.
Enyi maweza yote ya Bwana, mtukuzeni Bwana;
msifuni na kumtukuza milele. K.
Enyi jua na mwezi, mtukuzeni Bwana;
msifuni na kumtukuza milele. K.
SHANGILIO LA INJILI
UFUNUO 2:10c
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Uwe mwaminifu hata kufa, asema Bwana, nami nitakupa taji la uzima.
Aleluya.
INJILI
Luka 21:5—11
Wakati ule: Baadhi ya watu waliongelea habari za hekalu, hasa mawe mazuri na mapambo ya wakfu. Yesu akasema, "Haya yote mnayoyaona, siku zitakuja ambapo jiwe halitaachwa juu ya jiwe. Yote yatabomolewa." Wakamwuliza wakisema, "Mwalimu, hayo yatakuwa lini? Na iko ishara gani inayodokeza mwanzo wa kutimia hayo?" Akasema, "Angalieni msije mkadanganywa, kwa maana wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, 'Mimi ndiye,' tena 'Wakati umewadia.' Msiwafuate hao. Mtakaposikia habari za vita na misukosuko, msihangaike, kwa maana hayo hayana budi kutendeka kwanza, lakini si mwisho bado." Kisha akawaambia, "Taifa litashambulia taifa, na ufalme utashambulia ufalme. Kutakuwa na matetemeko makubwa ya nchi huko na huko, na maradhi na njaa na matisho na ishara kubwa kutoka uwinguni."
Injili ya Bwana.