SOMO 1
Danieli 1:1—6, 8—20
Katika mwaka wa tatu wa utawala wake Yehoiakimu, mfalme wa Yuda, Nebukadneza, mfalme wa Babiloni, aliufikia Yerusalemu akaushambulia. Bwana akamtoa Yehoiakimu, mfalme wa Yuda, na sehemu ya vyombo vya nyumba ya Mungu, mikononi mwa mfalme wa Babiloni, aliyevichukua mpaka nchi ya Shinari, mpaka nyumba ya miungu yake, akaviweka katika nyumba ya hazina ya miungu yake. Mfalme akamwambia Ashpenazi, mkuu wa watumishi wake, alete vijana wengine kati ya Waisraeli, wa ukoo wa kifalme au wa uzao wa wenye cheo bora. Wawe vijana wasio na upungufu, wazuri wa sura, wajuzi wa hekima yote, hodari kwa ufahamu, wenye elimu na akili, na ambao wangeweza kutumika katika nyumba ya mfalme; naye mkuu wa watumishi awafundishe mwandiko na lugha ya Wakaldayo. Mfalme akawaandikia kwa kila siku posho ya chakula cha mfalme na ya divai aliyokunywa. Akaagiza wafundishwe hivyo muda wa miaka mitatu, ili baadaye wamtumikie mfalme. Kati ya vijana hao walikuwapo Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria, walio wa kabila la Yuda. Naye Danieli akakusudia moyoni mwake, ya kuwa hatachafuka kwa kula chakula cha mfalme wala kunywa divai aliyokunywa. Basi akamwomba yule mkuu wa watumishi ruhusa ili asijichafue. Mungu akamjalia Danieli neema na fadhila machoni pa yule mkuu wa watumishi. Lakini yule mkuu wa watumishi akamwambia Danieli, "Namwogopa bwana wangu mfalme, aliyewaandikia ninyi chakula chenu na kinywaji chenu. Ikiwa ataona nyuso zenu zimekonda zaidi kuliko nyuso za vijana wengine wa umri wenu, mtakitia kichwa changu hatarini mbele ya mfalme." Danieli akamwambia msimamizi aliyewekwa na mkuu wa watumishi, ili awatunze Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria, "Utujaribu basi watumishi wako muda wa siku kumi. Tupewe mboga tule, na maji tunywe. Utatazama sura zetu na sura za vijana wale wanaokula chakula cha mfalme, nawe utatutendea sisi watumishi wako kadiri utakavyoona." Yule msimamizi akakubali ombi lao akawajaribu muda wa siku kumi; mwisho wa siku zile kumi, wakaonekana kuwa na sura nzuri zaidi na wenye kunenepa zaidi kuliko vijana wote waliokula chakula cha mfalme. Tangu hapo, msimamizi yule akaendelea kuondoa kile chakula na divai waliyopewa wanywe, akawapa mboga. Mungu akawajalia vijana wale wanne akili na elimu ya mwandiko wote na hekima, naye Danieli akajaliwa na ufahamu wa maono na ndoto yoyote. Mwisho wa zile siku alizoweka mfalme ili waletwe kwake, yule mkuu wa watumishi akawaleta wale vijana mbele ya mfalme Nebukadneza. Naye mfalme akaongea nao, na kati yao hakupatikana aliye sawa na Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria; nao wakaingia kumtumikia mfalme. Na katika kila swali lenye kuomba hekima na akili alilowauliza mfalme, aliwaona wao bora mara kumi zaidi kuwapita waaguzi na wacheza mazingaombwe wa ufalme wake mzima.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
DANIELI 3:29—30, 31, 33, 32, 34 (K. 29b) [au: NV 3:52, 53, 54, 55, 56 (K. 52b)]
K. Usifiwe na utukuzwe milele!
Uhimidiwe, ee Bwana, Mungu wa baba zetu,
usifiwe, na utukuzwe milele;
litukuzwe jina lako tukufu na takatifu,
lisifiwe na litukuzwe milele. K.
Utukuzwe katika hekalu la utukufu wako mtakatifu,
unastahili sifa na utukufu juu ya yote milele. K.
Utukuzwe katika kiti cha ufalme wako
unastahili sifa na kuinuliwa juu ya yote milele. K.
Utukuzwe, ewe unayepima vilindi, ukaaye juu ya makerubi,
unastahili sifa na kuinuliwa juu ya yote milele. K.
Utukuzwe katika nguvu zote za mbinguni,
uimbiwe na kutukuzwa milele. K.
SHANGILIO LA INJILI
MATHAYO 24:42a, 44
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Kesheni na muwe tayari, kwa maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoidhania.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 21:1—4
Wakati ule: Yesu aliinua macho, akawaona matajiri wakitia zaka zao katika sanduku la mchango. Akamwona pia mjane maskini akitia humo sarafu mbili. Akasema, "Amin, nawaambieni, huyu mjane fukara ametia zaidi kuliko wote. Maana hao wote walitia katika sanduku iliyozidi katika mali yao, bali huyu, katika ufukara wake, ametia yote aliyokuwa nayo."
Injili ya Bwana.