SOMO 1
Ezekieli 34:11—12, 15—17
Bwana Mungu asema hivi: Tazama! Mimi mwenyewe nitashughulika na kondoo wangu, nami nitawachunga. Kama vile mchungaji anavyochunga kundi lake, akiwa kati ya kondoo wake waliotawanyika, vivyo hivyo mimi nitawachunga kondoo wangu. Nitawaokoa kutoka kote walikotawanywa nyakati za wingu jeusi. Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo wangu, nami nitawalaza — asema Bwana. Nitamtafuta kondoo aliyepotea, nitamrudisha yule aliyebaki nyuma, nitamfungia vitambaa aliyeumizwa, nitamtia nguvu aliye mgonjwa; nitamwangamiza aliye mnono na mwenye nguvu, nitawalisha kwa haki. Nanyi, enyi kondoo wangu, Bwana Mungu asema: Tazameni, nitahukumu kati ya kondoo na kondoo, kati ya kondoo dume na mabeberu.
Neno la Bwana .
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 23:1—2a, 2b—3, 5—6 (K. 1)
K. Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu.
Bwana ndiye mchungaji wangu,
sitapungukiwa na kitu.
Hunipumzisha katika malisho mabichi. K.
Hunipeleka kwenye maji matulivu;
hunipatia nguvu.
Huniongoza katika njia zilizo sawa
Kwa ajili ya jina lake. K.
Waandaa meza mbele yangu,
machines pa adui zangu;
umenipaka mafuta kichwani;
kikombe changu kinafurika. K.
Kweli, wema na fadhili zitanifuata
siku zote za maisha yangu;
na nitakaa nyumbani mwa Bwana
kwa miaka mingi ijayo. K.
SOMO 2
1 Wakorintho 15:20—26, 28
Ndugu zangu: Kristo amefufuka katika wafu kama malimbuko ya wenye kulala. Kwa maana mauti imeletwa na mtu mmoja, na ufufuko wa wafu umeletwa pia na mtu mmoja. Kama wote hufa katika Adamu, vilevile wote watapata tena uzima katika Kristo. Lakini kila mmoja kwa zamu yake; wa kwanza ni Kristo; baadaye walio wa Kristo siku ya tokeo lake. Hapo ndipo mwisho: atakapokuwa anampa Mungu Baba ufalme baada ya kuangamiza kila utawala, na kila mamlaka, na kila enzi. Maana sharti awe mfalme hata awaweke maadui wote chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni mauti. Baada ya kuwekwa yote chini yake, naye Mwana mwenyewe atajiweka chini yake yeye aliyemwekea yote chini yake, ili Mungu awe yote katika yote.
Neno la Bwana.
SHANGILIO LA INJILI
MARKO 11:9, 10
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mbarikiwa anayekuja kwa jina la Bwana! Umebarikiwa ufalme ujao wa baba yetu Daudi!
W. Aleluya.
INJILI
Mathayo 25:31—46
Wakati ule: Yesu aliwaambia wafuasi wake: "Atakapokuja Mwana wa Mtu katika utukufu wake na malaika wote pamoja naye, ataketi katika kiti cha utukufu wake. Na mataifa yote yatakusanywa mbele yake, atawatenganisha watu kama vile mchungaji anavyowatenganisha kondoo na mbuzi. Atawaweka kondoo upande wake wa kulia, na mbuzi upande wake wa kushoto. Halafu mfalme atawaambia wale wa kulia kwake, 'Njooni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu. Urithini ufalme mliowekewa tangu mwanzo wa dunia. Kwa maana nalikuwa na njaa, mkanilisha, nalikuwa na kiu mkaninywesha, nalikuwa mgeni mkanikaribisha, nalikuwa uchi mkanivisha, nalikuwa mgonjwa mkaja kunitazama, nalikuwa kifungoni mkaja kuniona. Hapo waadilifu watamjibu na kusema, 'Bwana, lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Lini tulikuona u mgonjwa au kifungoni, tukaja kukuona?' Mfalme atawajibu, 'Amin, nawaambieni, mliyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.' Kisha atawaambia na wale wa kushoto, 'Ondokeni kwangu ninyi walaaniwa, nendeni katika moto wa milele uliowekwa tayari kwa Shetani na malaika wake. Kwa maana nalikuwa na njaa, hamkunilisha: nalikuwa na kiu, hamkuninywesha. Nalikuwa mgeni, hamkunikaribisha; nalikuwa uchi, hamkunivisha; nalikuwa mgonjwa na kifungoni, hamkunitazama.' Hapo wao pia watajibu na kusema, 'Bwana, lini tulipokuona una njaa, au kiu, au mgeni, au huna nguo, au u mgonjwa, au kifungoni tusikutumikie?' Naye atawajibu, 'Amin, nawaambieni, mlipokataa kumtendea mmojawapo katika hawa wadogo, mlikataa kunitendea mimi.' Na hao wataingia katika adhabu ya milele; bali waadilifu wataingia katika uzima wa milele."
Injili ya Bwana.