SOMO 1
1 Wamakabayo 6:1—13
Siku zile: Mfalme Antiokusi alipita katika mikoa ya mashariki, hapo akasikia habari za Elamu, mji wa Uajemi, uliosifiwa sana sababu ya utajiri wake wa fedha na dhahabu yake, na kuwa hekalu la mji huo lilikuwa na mali nyingi, na humo mlikuwa na ngao za dhahabu, na mavazi ya vita na silaha, alizoacha Aleksanda, mwana wa Filipo, na mfalme wa Masedonia, aliyekuwa wa kwanza mwenye kuwatawala Wagiriki. Basi mfalme Antiokusi akauendea ule mji, akataka kuukamata na kuutwaa mateka. Lakini akashindwa kutenda vile, kwa sababu wenyeji wa mji ule walipashwa habari ya kusudi lake, wakashindana naye na kufanya vita. Naye akakimbia akaondoka kwa moyo wenye huzuni kuu kurudi Babiloni. Alipokuwa bado katika Uajemi, akapashwa habari ya kwamba majeshi yake yaliyokwenda kupigana katika nchi ya Yuda wameshindwa. Lisiasi alikuwa amekwenda huko na jeshi la nguvu sana, lakini amekimbizwa na Wayahudi; nao Wayahudi wamepata nguvu zaidi, kwa sababu wamechukua mateka ya majeshi walioshindwa nao, mateka ya silaha na wafungwa na mali nyingi; nao wamebomoa lile chukizo lililojengwa na mfalme juu ya altare huko Yerusalemu; wakajenga tena kuta ndefu zenye kuzunguka patakatifu kama zamani, na Beth-zuri pia, mji wake mfalme. Alipopata habari hiyo, mfalme Antiokusi akahuzunika sana akashtuka kabisa. Akajilaza kitandani akawa mgonjwa kwa huzuni, kwa sababu mambo hayakutukia alivyotamani. Akalala huko siku nyingi, kwa sababu alisongwa na huzuni kubwa, hata akadhani kwamba atakufa. Akawaita rafiki zake wote, akawaambia, "Usingizi umejitenga mbali macho yangu, na moyo wangu umevunjika kwa taabu. Nikasema moyoni mwangu, 'Nimesongwa na huzuni kubwa, nami nimezama katika taabu kubwa kabisa! Mimi nilikuwa bora na mwenye kupendwa wakati nilipokuwa na uwezo.' Lakini sasa ninayakumbuka mabaya niliyofanya huko Yerusalemu, nilipotwaa vyombo vyote vya fedha na dhahabu, nikawaangamiza wakaaji wote wa Yuda bila sababu. Ninaungama ya kuwa kwa sababu hiyo nimepata misiba hiyo; na tazameni, ninakufa kwa huzuni kuu katika nchi ya kigeni."
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 9:2—3, 4 na 6, 16b na 19
K. Nitaufurahia wokovu wako, ee Bwana.
Nitakutukuza, ee Bwana, kwa moyo wangu wote;
nitayashuhudia matendo yako ya ajabu.
Kwa furaha nitakushangilia wewe,
nitaliimbia jina lako wewe, Uliye Juu. K.
Kwa kuwa adui zangu wanavyorudi nyuma,
jinsi wanavyojikwaa na kuangamia mbele yako.
Umewapatiliza mataifa, umewaangamiza waovu,
umelifuta jina lao milele na milele. K.
Mguu wa mataifa umenaswa kwa wavu waliouficha.
Lakini maskini hatasahauliwa daima,
matumaini ya wanyonge hayatapotea milele. K.
SHANGILIO LA INJILI
2 Timotheo 1:10
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mwokozi wetu Kristo Yesu ameyashinda mauti, na ametangaza uzima wa milele kwa njia ya Injili.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 20:27—40
Wakati ule: Walikuja baadhi ya Masadukayo, ndio watu wanaokana ufufuko wa wafu, wakamwuliza Yesu swali hili, "Mwalimu, Musa ametuandikia hivi, 'Mtu akifiwa na ndugu mwenye mke pasipo watoto, sharti mtu huyo amchukue mke wa ndugu yake amzalie ndugu yake mtoto.' Basi, kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza alioa, akafa bila mtoto. Wa pili kadhalika. Wa tatu pia akamwoa. Na vivyo hivyo wote saba, wakafa bila kuacha mtoto. Mwisho mwanamke akafa pia. Hapo wakati wa ufufuko mwanamke huyo atakuwa mke wa nani kati ya hao? Kwa maana aliolewa na wote saba." Yesu akawaambia, "Wana wa dunia hii huoa n huolewa. Lakini wale wajaliwao kushiriki uzima wa milele na ufufuko katika wafu, hawaoi wala hawaolewi. Kwa maana hawawezi kufa tena, kwani ni kama malaika, wao ni wana wa Mungu, kwa sababu ni wana wa ufufuko. Ya kuwa wafu hufufuka, hata Musa alionyesha katika masimulizi ya kichaka. Hapo alipomtaja Bwana kuwa Mungu wa Abrahamu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Kwani Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai, maana kwa sababu yake wote wanaishi." Baadhi ya Waandishi wakajibu na kumwambia," Mwalimu, umesema vema." Baadhi ya hayo hawakuthubutu tena kumwuliza neno.
Injili ya Bwana.