SOMO 1
1 Wamakabayo 4:36—37, 52—59
Siku zile: Yuda na ndugu zake walisemezana, "Maadui wetu wameshindwa, imetupasa sasa kuondosha uchafu wa hekalu na kuliweka wakfu tena." Askari wote wa majeshi wakaenda kwa makundi kwa mlima wa Sioni. Siku ya ishirini na tano ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa mia moja arobaini na nane, walitolea sadaka, kama ilivyoamriwa katika Sheria, juu ya altare mpya ya sadaka za kuteketezwa waliyoijenga. Wakati ule ule na siku ile ile watu wa mataifa walipoichafua altare, siku ile ile ilibarikiwa tena na Wayahudi wenye kuimba nyimbo na kupiga vinubi, vinanda n matoazi. Watu wote wakaanguka kifudifudi, wakaabudu na kumsifu Mungu aliyewapa ushindi. Wakafanya sikukuu ya kutabarukiwa altare, muda wa siku nane, na kwa furaha wakatolea sadaka za kuteketezwa, na sadaka za kumsifu Mungu na kuomba amani. Wakapamba ukuta wa mbele ya hekalu kwa taji za dhahabu na ngao; wakatengeneza uwanja na nyumba zake, wakaviwekea milango. Kukawa na furaha kubwa sana kati ya watu, wakaondoa ile haya iliyoletwa na watu wa mataifa. Yuda na ndugu zake na mkutano wote wa Israeli wakakusudia ya kwamba siku za kutabarukiwa altare zitaadhimishwa kwa furaha na shangwe kila mwaka, wakati huo huo, muda wa siku nane, tangu siku ya ishirini na tano ya mwezi wa tisa.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
1 Mambo Ya Nyakati 29:10, 11abc, 11d-12a, 12bcd
K. Tunausifu utukufu wa jina lako, ee Bwana.
Utukuzwe, ee Bwana,
Mungu wa Israeli baba yetu,
milele hata milele. K.
Ukuu ni wako, ee Bwana, na uweza,
na utukufu, na kushindana na enzi;
maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako. K.
Ee Bwana, ufalme ni wako.
Nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote.
Utajiri na heshima hutoka kwako. K.
Nawe unatawala juu ya yote.
Na mkononi mwako mna uweza na nguvu;
tena mkononi mna kuwatukuza na kuwawezesha wote. K.
SHANGILIO LA INJILI
YOHANE 10:27
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Kondoo wangu huisikia sauti yangu, asema Bwana; nami nawajua, nao wanifuata.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 19:45—48
Wakati ule: Yesu aliingia hekaluni, akaanza kuwafukuza wenye kuuza humo, akawaambia, "Imeandikwa, 'Nyumba yangu ni nyumba ya sala,' lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi." Akawafundisha kila siku hekaluni. Hapo makuhani wakuu na Waandishi pamoja na viongozi wa watu wakatafuta nafasi ya kumwangamiza, lakini hawakuona njia ya kutimiza azimio lao, kwa sababu watu wote waliambatana naye na kumsikiliza.
Injili ya Bwana.