SOMO 1
1 Wamakabayo 2:15—29
Siku zile: Wajumbe wa mfalme, wenye kazi ya kuwashurutisha watu kuacha dini yao, walifika Modini siku moja, wakataka wenyeji watolee sadaka ya kishenzi. Waisraeli wengi wakakubali wakaandamana nao, lakini Matathia na wanawe wakajitenga kando, pamoja. Wajumbe wa mfalme wakamwambia Matathia, "Wewe u mkubwa hapa, u mtu wa maana wa mji huu, na wana wako na jamaa hufuatana nawe. Basi, imekupasa wewe kwanza ushike amri ya mfalme, ufanye anavyotaka, ndivyo watu wa makabila mengine walivyofanya, nao maafisa wa Yuda vile vile, nao wengine wote tuliowaacha Yerusalemu. Utakuwa mmojawapo wa rafiki zake mfalme na wana wako, mtasifiwa sana na kupewa zawadi nyingi na vyombo vya fedha na vya dhahabu." Lakini Matathia akajibu kwa sauti kuu, "Hata kama mataifa yote ya umilki wake mfalme wangeacha dini ya mababu zao na kumtii mfalme kwa kufuata amri hizo, sisi tutakaa imara katika maagano ya baba zetu, mimi mwenyewe na wana wangu na jamaa zangu pia: sisi wote. Mbingu zitushuhudie kama tutaziacha sheria na amri. Sisi tunakataa kushika amri hizo za mfalme; hatuachi dini yetu, hata kwa kiasi kidogo." Alipomaliza maneno hayo Myahudi mmoja akatokea mbele ya watu, akitaka kutoa sadaka katika altare ya Modini, ilivyokuwa amri ya mfalme. Hapo Matathia akashika hasira kubwa, akatetemeka mwili wake wote; akamrukia mtu yule, akampiga, akamuua palepale mbele ya altare. Akampiga pia mjumbe wa mfalme aliyetaka kumshurutisha atoe sadaka, akamuua vile vile. Kisha akaibomoa altare yenyewe. Juhudi aliyokuwa nayo ikafanana na bidii ya yule Finehasi aliyempiga Zimri mwana wa Salu. Matathia akatangaza kote mjini kwa sauti kuu, "Kila mmoja apendaye Sheria na kushika agano, ashirikiane nami!" Halafu yeye na wanawe wakatoroka wakajificha milimani, wakaacha mali yao yote mjini. Wenyeji wengi wenye kuipenda Sheria na kutafuta haki, wakaenda nao kukaa jangwani.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 50:1—2, 5—6, 14—15 (K. 23bc)
K. Aendaye bila hatia, nitamwonyesha wokovu wa Mungu.
Mwenyezi, Mungu Bwana ananena,
anaita dunia toka maawio ya jua / mpaka machweo yake.
Mungu anang'ara kutoka Sioni,
mji wa uzuri kamili. K.
Wakusanyeni kwangu waamini wangu,
waliofunga nami agano kwa sadaka.
Mbingu zatangaza haki yake,
maana Mungu ataisalimisha ndiye mwamuzi. K.
Umtolee Mungu dhabihu za shukrani;
umtimizie Aliye Juu nadhiri zako.
Uniite siku ya taabu,
nitakuopoa, nawe utanisifu. K.
SHANGILIO LA INJILI
TAZAMA ZABURI 95:7d, 8a
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake, msiifanye migumu mioyo yenu.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 19:41—44
Wakati ule: Yesu alipokaribia zaidi kuuona mji wa Yerusalemu, aliulilia machozi, akisema, "Laiti ungalitambua siku ya leo yale yaletayo amani! Lakini sasa yamefumbwa machoni mwako. Kwa maana siku zitakuja, ambapo adui zako watachimba handaki pande zako zote; watakuzingira, watakusonga toka pande zote. Watakuangusha chini wewe na watoto wako walio ndani yako, na hawatakuachia jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukuutambua wakati wa kujiliwa kwako."
Injili ya Bwana.