SOMO 1
2 Wamakabayo 7:1, 20—31
Siku zile: Ilitukia kwamba ndugu saba walikamatwa pamoja na mama yao, mfalme alitaka kuwashurutisha kula nyama ya nguruwe inayokatazwa katika sheria ya Mungu na akawapiga mijeledi na kuwatesa. Hasa mama yao ndiye anayestahili sifa zetu, hata tukumbuke uhodari wake kwa heshima. Kwa siku moja tu aliwaona watoto wake wote wakiuawa, akavumilia bila kulegea jinsi alivyokuwa akimtegemea Bwana wake. Akawapa moyo watoto wake wote, kila mmoja, kwa lugha yao ya asili, yeye mwenyewe akajaa moyoni hekima akajitia nguvu ya kiume ijapo mwanamke. Akawaambia, "Sijui namna gani mlitungwa tumboni mwangu. Si mimi niliyewapa roho na uzima, wala si mimi niliyepanga sehemu za mwili wa kila mmoja wenu. Bali ni yeye, Muumba wa ulimwengu, anayemuumba mwanadamu tangu asili yake, na kuisimamia asili ya viumbe vyote, naye katika huruma yake atawarudishia ninyi roho na uzima, kwa sababu sasa mnajidharau wenyewe kwa ajili ya sheria zake." Mfalme Antiokusi akadhani kuwa amedharauliwa, akajiona kama ametukanwa kwa maneno hayo. Lakini mfalme alimwambia yule aliye mdogo katika hao ndugu maneno ya kumbembeleza, hata alimwahidia kwa kiapo ya kwamba atamfanya kuwa tajiri na mwenye heri, akiziacha desturi za baba zake; akaongeza ya kuwa atamfanya kuwa rafiki yake, na kumweka katika daraja ya uwezo juu ya watu. Lakini yule kijana hakukubali maneno yake hata kidogo, basi mfalme akamwuliza mama yake kijana huyo, ili amshauri mtoto wake ajiokoe. Akamwomba hivi mara nyingi, hata mwisho yule mama akakubali kumshauri mtoto wake. Yule mama akamwinamia mtoto, lakini alimfanyia mzaha yule mfalme mkorofi, akamwambia mtoto hivi kwa lugha ya baba zake, "Mwanangu, unihurumie mimi niliyekuchukua tumboni muda wa miezi tisa, na kukunyonyesha muda wa miaka mitatu, na kukulisha na kukutunza na kukupatia vyote vya lazima, upate kuufikia umri wako wa sasa. Nakusihi, mwanangu, inua macho yako utazame mbingu na dunia, ukaangalie vyote vilivyomo; ukatambue ya kwamba Mungu ameumba hivyo vyote bila kutumia vitu vilivyokuwako kabla, naye amewaumba wanadamu kwa namna hiyo hiyo. Usimwogope yule mtesaji, lakini ujionyeshe hodari sawasawa na ndugu zako, ukubali kufa, ili kwa huruma yake Mungu nipate kukuona tena pamoja na ndugu zako." Yule mama alipomaliza maneno yake, yule kijana akasema, "Je, mnangoja nini? Mimi siitii amri ya mfalme, bali naitii amri ya sheria waliyopewa baba zetu kwa njia ya Musa. Nawe uliyetunga kila namna ya mabaya juu ya Waebrania, hutapona hata kidogo katika mikono ya Mungu."
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 17:1, 5—6, 8 na 15 (K. 15b)
K. Niamkapo, nishibe kwa kuuona uso wako, ee Bwana.
Usikie, ee Bwana, ombi langu la haki,
usikilize kilio changu,
uitegee sikio sala yangu:
itokayo katika midomo isiyo na udanganyifu. K.
Nimedumisha hatua zangu katika njia zako.
Miguu yangu haikutetereka.
Mimi nakuita; uniitikie, ee Mungu.
Unielekezee sikio lako, usikie ombi langu. K.
Unilinde kama mboni ya jicho lako.
Unifiche kivulini mwa mbawa zako.
Nami, nipate zawadi ya kuwa mwenye haki, kuuona uso wako;
niamkapo, nishibe kwa kuiona sura yako. K.
SHANGILIO LA INJILI
TAZAMA YOHANE 15:16
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mimi niliwachagua ninyi, kusudi mwende kuzaa matunda, na matunda yenu yadumu, asema Bwana.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 19:11—28
Wakati ule: Yesu alisimulia mfano kwa maana alikuwa karibu na Yerusalemu, na watu wake walidhani kwamba ufalme wa Mungu utatokea pale pale. Basi, alisema, "Mtu mwenye cheo tangu kuzaliwa alisafiri aende katika nchi ya mbali kusudi ajipatie ufalme na kurudi tena. Akawaita watumishi wake kumi, akawapa mina kumi za fedha, akawaambia, 'Fanyeni biashara hata nitakaporudi.' Lakini raia wake walimchukia, wakatuma wajumbe wamfuate na kusema, 'Hatumtaki huyu kuwa mfalme wetu.' Baada ya kupata ufalme akarudi, akaamuru wale watumishi aliowapa fedha waitwe, apate kuijua biashara aliyofanya kila mmoja. Akaja wa kwanza akasema, 'Bwana, mina yako imeleta faida ya mina kumi.' Akamwambia, 'Vema, mtumishi mwema! Kwa kuwa umekuwa mwaminifu katika jambo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi.' akaja wa pili, akasema, 'Bwana, mina yako imeleta mina nyingine tano.' akamwambia huyu pia, 'Nawe uwe na mamlaka juu ya miji mitano.' Akaja mwingine, akasema, 'Bwana, tazama mina yako; nimeitunza katika leso, kwa maana nilikuogopa, kwa sababu wewe ni mtu mkali, wachukua usichokiweka akiba; wavuna usipopanda." Akamwambia, 'Nitakuhukumu kutokana na kauli yako, ewe mtumishi mbaya. Umejua kwamba mimi ni mtu mkali nichukuaye nisichoweka akiba na kuvuna nisichopanda; mbona hukuweka fedha yangu benki? Baada ya kurudi ningaliweza kuichukua pamoja na faida yake." Akawaambia wale waliosimama pale, 'Ichukueni mina yake, mkampe yule mwenye mina kumi.' Wakamwambia, 'Bwana, anazo mina kumi.' Nawaambieni, kila mwenye kitu atapewa, bali asiye na kitu atapokonywa hata kile alicho nacho. Lakini wale adui zangu wasiotaka niwe mfalme wao waleteni hapa, muwaue mbele yangu." Baada ya maneno hayo, Yesu alitangulia kwenda Yerusalemu.
Injili ya Bwana.