SOMO 1
2 Wamakabayo 6:18—31
Siku zile: Eleazari alikuwa mkuu mmoja wa kwanza kati ya walimu wengine wote wa Sheria, mtu aliyekwisha kuzeeka kweli, umbo lake la kuomba heshima, nao walitaka kumshurutisha ale nyama ya nguruwe, hata wakamfunua mdomo kwa nguvu. Lakini, akiona ni afadhali kufa na heshima kuliko kukaa mzima kwa fedheha, alikubali kwenda kupigwa mijeledi, akaitema nyama ile, ilivyompasa mtu mwenye moyo wa kukataa chakula chenye kukatazwa, hata kwa hatari ya uzima. Watu walioandaa karamu ile ya kishenzi wakamchukua kwa faragha, kwa kuwa mzee yule alikuwa rafiki yao tangu zamani, wakamwambia kwamba wataleta nyama nyingine atakayoweza kula ila ajisingizie tu kwamba anakula nyama ya sadaka, ilivyokuwa amri ya mfalme. Akifanya namna hiyo angeweza kuepa kuuawa na kufaidi kwa ajili ya urafiki wa siku nyingi waliokuwa nao. Lakini yeye alikata shauri mwenyewe kwa namna iliyofaa kwa umri wake, na kwa hekima ya uzee na ya mvi zake alizopata kwa kazi ya heshima na kwa uadilifu wa moyo ulioonekana katika mwendo wake tangu utoto. Hasa alitaka kushika imara sheria ile iliyowekwa na Mungu mwenyewe. Basi akasema upesi, "Afadhali mnipeleke kaburini." Akaongeza, "Mtu akiwa mzee kama mimi hafai kujisingizia; vijana wengi watafikiri kwamba Eleazari amekubali kufuata dini za kigeni alipokuwa mzee wa miaka tisini. Na kwa ajili ya masingizio hayo, wataongozwa vibaya, na na litakuwa kosa langu, nililotenda ili kuongeza siku chache za maisha yangu. Uzee wangu utapata haya na fedheha kubwa. Juu ya hayo, nikiepuka adhabu ya binadamu sasa, lakini kisasi cha Mungu Mwenyezi siwezi kukiepuka, sasa na baada ya kufa. Ndiyo maana ikiwa nakubali kutoa uzima wangu bila hofu, nitakuwa mtu niliyestahili kuona uzee wangu kweli, nao vijana watapata kuona mfano mzuri wa kifo hodari, nilichopokea kwa moyo wangu wote na kwa furaha, kuliko kuidharau sheria tukufu ya Torati takatifu." Alipomaliza maneno hayo alipelekwa kuuawa bila kukawia. Wakamtenda ukali mkubwa sana kwa ajili ya maneno aliyosema, watu wale waliotaka kumhurumia kwanza waligeuza upole kuwa ukali. Wakaona maneno yake ni ukorofi. Kwa sababu ya kupigwa hakukawia kukaribia saa ya kufa, na akasema kwa sauti inayofifia, "Bwana ajuaye yote, anafahamu kwamba nateswa vibaya sana mwilini mwangu kwa kupigwa vikali hivi; ingawa ningaliweza kuepa kifo hiki, lakini moyoni mwangu napokea madhulumu hayo kwa furaha, kwa sababu namheshimu Mungu." Ndivyo alivyofariki. Kwa jinsi alivyomaliza maisha yake akawapa vijana na wengine wote wa taifa letu mfano mzuri wa uhodari na wa uadilifu tuwezao kukumbuka.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 3:2—3, 4—5, 6—7 (K. 6b)
K. Bwana ndiye anayenitegemeza.
Ee Bwana, wanaonisonga ni wengi!
Ni wengi wenye kunishambulia!
Ni wengi wenye kusema juu yangu,
"Huyu hapati wokovu kwa Mungu." K.
Lakini wewe, ee Bwana, ndiwe ngao yangu,
utukufu wangu, unayeinua kichwa changu.
Nilimlilia Bwana kwa sauti kubwa,
naye akaniitikia toka mlima wake mtakatifu. K.
Nilijilaza nikapata usingizi,
nikaamka kwa kuwa Bwana ananitegemeza.
Sitayaogopa maelfu ya watu
waliojipanga pande zote dhidi yangu. K.
SHANGILIO LA INJILI
1 YOHANE 4:10b
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mungu alitupenda hata akamtuma Mwanaye awe malipizi kwa dhambi zetu.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 19:1—10
Wakati ule: Yesu aliingia Yeriko akapita katikati yake. Pale palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, naye alikuwa mtoza ushuru mkuu, tena mtu tajiri. Alitafuta nafasi ya kumwona Yesu apate kumfahamu ni nani; lakini alishindwa kwa sababu ya umati wa watu, maana alikuwa mfupi. Akatangulia mbio, akakwea mkuyu apate kumwona kwa maana njia ilipita huko. Yesu alipofika pale, alitazama juu, akamwambia, "Zakayo, shuka upesi, kwa maana leo imenipasa kushinda nyumbani mwako." Akashuka upesi, akampokea kwa furaha. Wote wenye kuona hayo walinung'unika wakisema, "Amekwenda kushinda kwa mkosefu." Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, "Sikiliza, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na kama nimemnyang'anya mtu kitu nitamrudishia mara nne." Yesu akawaambia, "Leo wokovu umefikia nyumba hii, kwa kuwa huyu pia ni mwana wa Abrahamu. Kwa maana Mwana wa Mtu amekuja kutafuta na kuokoa kilichopotea."
Injili ya Bwana.