SOMO 1
1 Wamakabayo 1:10-15, 41-43, 54-57, 62-64
Siku zile: Mtu mmoja alitokea, mzaliwa wa upotovu kweli, jina lake Antiokusi Epifanesi, mwana wa mfalme Antiokusi. Kwanza alikaa Roma kama mfungwa wa amana. Halafu akapata ufalme mwaka wa mia moja thelathini na saba wa utawala wa Wagiriki. Kulikuwa na wana uovu katika nchi ya Israeli siku zile waliofanya bidii ya kuwaharibu Wayahudi wengi wakisema, "Twende tufanye maagano na mataifa wanaotuzunguka; kwa maana tangu tulipoacha kuwa rafiki zao misiba ya kila namna imetuangukia." Maneno hayo yakapendeza; baadhi ya wenyeji wakakubali hima kumwendea mfalme, wakapatana naye kuzishika desturi za watu wa mataifa. Pale Yerusalemu walijenga ukumbi kulingana na utamaduni wa watu wa mataifa. Wakajifanya kama hawakutahiriwa, wakakanusha agano takatifu; wapate kushirikiana na watu wa mataifa; namna hiyo wakajiuza dhambini. Ndipo mfalme Antiokusi alipotangaza amri mpya kwa nchi zote za milki yake, kwamba ni lazima watu wote waunganike kuwa taifa moja tu, kila kabila likipaswa kuziacha desturi zake. Basi, makabila mengine yakakubali amri hiyo ya mfalme, na kati ya Waisraeli walikuwako wengi waliopendezwa na dini mpya; wakakubali kutolea sadaka za miungu na hata Sabato wakaidharau. Siku ya kumi na tano ya mwezi wa Kislevu, ya mwaka mia moja arobaini na tano, wakatia chukizo la uharibifu katika altare ya sadaka, na katika miji mingine ya Yuda altare nyingine zikajengwa. Na barabarani mbele ya nyumba wakafanya sadaka za mafukizo. Vitabu vyote vya sheria vilivyopatikana vikararuliwa na kuchomwa moto. Na mtu ambaye nyumbani mwake kitabu cha agano kilipatikana, au yeye aliyezidi bado kuishika Sheria, aliuawa kwa amri ya mfalme. Lakini ingawa masumbuko yalikuwa mengi mno, Waisraeli wengi walikuwa imara na waaminifu bila kulegea mioyoni mwao, wakakataa kula vyakula najisi; wakaona ni afadhali kufa kuliko kuchafuka kwa vyakula, na kudharau sheria takatifu ya agano. Ghadhabu kali sana ilishuka juu ya Israeli.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 119:53, 61, 134, 150, 155, 158
K. Unijalie uzima, ee Bwana, nami nitazishika amri zako.
Ghadhabu imenishika sababu ya waovu
wanaoiacha sheria yako. K.
Kamba za waovu zimenifunga,
lakini sikuisahau sheria yako. K.
Uniopoe na dhuluma ya mwanadamu,
nipate kuzishika amri zako. K.
Wanaonifuata kwa njama mbaya, wamenikaribia;
wamejitenga mbali na sheria yako. K.
Wokovu uko mbali na watu waovu,
kwa kuwa hawazitafuti kanuni zako. K.
Nimewaona wasioamini nikachukizwa;
kwa maana hawakutii neno lako. K.
SHANGILIO LA INJILI
YOHANE 8:12
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana; anifuataye mimi atakuwa na nuru ya uzima.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 18:35—43
Yesu alipokaribia Yeriko, kulikuwa na mtu mmoja kipofu aliyekaa kando ya njia akiombaomba. Alipowasikia watu wanapita kwa wingi, aliuliza, "Kuna nini?" Wakamwambia, "Yesu wa Nazareti anapita." Akapaza sauti akisema, "Yesu, Mwana wa Daudi, unihurumie!" Wale waliotangulia wakamkemea anyamaze. Lakini yeye alizidi kuita, "Mwana wa Daudi, unihurumie!" Kisha Yesu akasimama, akaamuru aletwe kwake; alipomkaribia alimwuliza, "Ungependa nikufanyie nini?" Naye akasema, "Bwana, nipate kuona." Yesu akamwambia, 'Ona, imani yako imekuponya." Mara akaona, akamfuata akimtukuza Mungu. Na watu wote walipoona hayo walimsifu Mungu.
Injili ya Bwana.