SOMO 1
Hekima Ya Sulemani 18:14—16, 19:6—9
Ukimya mzito kabisa ulipozunguka kila kitu, na usiku ulipokuwa katikati ya mwendo wake, neno lako lenye kila uwezo kutoka mbinguni, kutoka kiti cha enzi cha kifalme, lilijirusha katikati ya nchi ile iliyopaswa kuangamizwa, kama mpiganaji mkali likichukua kama upanga mkali agizo lako lisilo na unafiki. Na kwa kusimama thabiti, likajaza mambo yote mauti, huku likizigusa mbingu, pia likitembea juu ya nchi. Maana, viumbe vyote, katika aina zake, vilipewa tena maumbile mapya; kwa kuyatumikia maagizo yako, kusudi watoto wako walindwe katika utulivu. Ulionekana uwingu wenye kutia kivuli kwenye makambi; na nchi kavu ikatokea pale palipokuwapo maji kwanza; na kutoka Bahari ya Shamu njia isiyo na kizuizi, na bonde lenye majani kutoka gharika ya kasi. Juu yake walipita kama taifa moja waliolindwa na mkono wako, wakitazama ishara za ajabu. Maana kama farasi walilishwa, na kama wanakondoo walirukaruka, wakakusifu wewe, Ee Bwana uliyewaokoa.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 105:2—3, 36—37, 42—43 (K. 5a)
K. Yakumbuke maajabu Bwana aliyoyatenda.
au: Aleluya.
Mwimbieni kwa ala za nyuzi;
elezeni matendo yake yote ya ajabu!
Lisifuni jina lake takatifu;
ufurahi moyo wa wenye kumtafuta Bwana! K.
Kisha akampiga kila mzaliwa wa kwanza katika nchi yao,
wazawa wa kwanza walio malimbuko ya nguvu yao ya uzazi.
Akawaondosha wakichukua fedha na dhahabu;
wala katika kabila yake hakuwepo aliyeyumba. K.
Maana alilikumbuka neno lake takatifu,
alilomwahidia Abrahamu, mtumishi wake.
Aliwaondosha taifa lake kwa furaha,
wateule wake kwa sauti za shangwe. K.
SHANGILIO LA INJILI
2 Wathesalonike 2:14
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mungu ametuita kwa njia ya Injili, ili tupate kuushiriki utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 18:1—8
Wakati ule: Yesu aliwafundisha makutano kwa mfano kuhusu umuhimu wa kusali daima bila kuchoka. Alisema, "Katika mji mmoja kulikuwa na hakimu asiyemcha Mungu wala kumjali mtu. Na katika mji huo kulikuwa na mama mjane, naye alimwendea tena na tena akisema, 'Nipatie haki kwa adui yangu.' Siku nyingi hakutaka, kisha akajiambia, 'Ingawa simchi Mungu wala simjali mtu, kwa kuwa mjane huyu ananisumbua nitahakikisha amepata haki yake, ama sivyo ataendelea kuja hadi amenichosha'" Bwana akaendelea kusema, "Sikilizeni asemayo hakimu mbaya. Na Mungu, je, hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku? Je, atakawia kuwasaidia? Nawaambieni, atawapatia haki upesi. Lakini Mwana wa Mtu atakapokuja, je, atapata imani duniani?"
Injili ya Bwana.