SOMO 1
Hekima Ya Sulemani 13:1—9
Watu wote kwa maumbile ni wa ubatili, watu ambao kutomjua Mungu kuliwaongoza; nao hawakuweza kumjua ambaye yupo, kwa njia ya mema yaliyopo mbele yao, wala kwa kuangalia kazi zake hawakumtambua yule fundi aliyezitenda. Lakini ama moto au upepo, ama hewa nyepesi au mzunguko wa nyota, ama maji ya kasi au mianga ya mbingu, walihesabu kuwa ndiyo miungu, inayotawala ulimwengu. Ikiwa walipendezwa na uzuri wa vitu hivyo, hata kudhani kwamba ni miungu, wajue jinsi alivyo bora zaidi Bwana, kuliko vitu hivyo; maana aliviumba muumbaji mwenyewe wa uzuri. Na ikiwa walishangazwa na nguvu na uwezo, waelewe kwa njia ya hivyo, jinsi alivyo na nguvu zaidi yule aliyeviumba. Maana, kutoka kwa ukubwa na uzuri wa viumbe inawezekana kumfahamu, kwa kulinganisha, yule aliyevifanya. Lakini, hata hivyo juu yao kuna kukaripiwa kidogo tu; kwa maana wanadanganyika kwa urahisi tu, maadamu wanamtafuta Mungu na kutaka kumwona. Maana, wanafanya upelelezi wakichunguza kwa bidii kazi zake, na wanaaminishwa kwa kuona jinsi vilivyo vizuri vitu wanavyovitazama. Lakini, wala hao hawastahili rehema. Maana, ikiwa walikuwa na uwezo wa kutambua kiasi hicho, wapate kufaulu kuyachunguza maisha ya ulimwengu, mbona hawakumtambua upesi Bwana mtawala wa vitu hivyo?
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 19:2—3, 4—5 (K. 2a)
K. Mbingu zinautangaza utukufu wa Mungu.
Mbingu zaeleza utukufu wa Mungu,
anga latangaza kazi ya mikono yake.
Mchana huupasha mchana habari hiyo,
nao usiku huujulisha usiku. K.
Hakuna neno, hakuna usemi,
wala sauti yake haisikiki;
lakini uvumi wake waenea duniani kote,
na maneno yake hata mipaka ya ulimwengu. K.
SHANGILIO LA INJILI
LUKA 21:28
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Tazameni juu, viinueni vichwa vyenu, kwa maana ukombozi wenu umekaribia.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 17:26—37
Wakati ule: Yesu aliwaambia wafuasi wake, "Kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa siku za Mwana wa Mtu; walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa mpaka siku Nuhu alipoingia katika safina, gharika ikaja, ikawaangamiza wote. Itakuwa sawa kama siku za Lutu: walikuwa wakila na kunywa, wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga; lakini siku ya Lutu alipotoka Sodoma, Mungu alinyesha moto na kiberiti kutoka mbinguni, zikawaangamiza wote. Ndivyo itakavyokuwa siku atakapotokea Mwana wa Mtu. Siku ile, aliye darini na riziki yake ndani ya nyumba, asishuke kuichukua, na kadhalika, aliye shambani asirudi nyumbani. Mkumbukeni mke wa Lutu. Kila anayejitahidi kuokoa nafsi yake, ataipoteza, na kila aipotezaye ataiokoa. Nawaambieni, usiku ule watu wawili watalala katika kitanda kimoja, mmoja atachukuliwa, na mwingine ataachwa. Wanawake wawili watakuwa wakisaga pamoja; mmoja atachukuliwa, na mwingine ataachwa. Watu wawili watakuwako shambani; mmoja atachukuliwa, na mwingine ataachwa." Hapo wakamwuliza, "Wapi, Bwana?" Akawaambia, "Kwenye mzoga, ndiko wanakokusanyika tai."
Injili ya Bwana.