SOMO 1
Hekima Ya Sulemani 7:22—8:1
Katika Hekima mna roho yenye akili, takatifu, pekee, yenye namna nyingi, nyepesi kuenea, nyepesi kwenda, yenye kupenya, isiyochafuka, wazi isiyoleta madhara, yenye kupenda wema, yenye umakinifu; bila kizuizi, yenye kutakia mema, yenye kupenda wanadamu, thabiti, imara, bila masumbuko, yenye kila uwezo, yenye kuangalia yote, yenye kupenya roho zote zenye akili, zilizo safi na nyepesi sana. Maana Hekima huenda upesi kuliko mwendo wowote, huingia na kupenya vyote kwa ajili ya usafi wake. Kwani ni pumzi ya uweza wa Mungu, na mmiminiko safi wa utukufu wa Mwenyezi; kwa hiyo chochote kilicho najisi hakiwezi kupenya ndani yake. Naam, ni mng'ao wa mwanga wa milele, na kioo kisicho na mawaa cha utendaji wa Mungu, na mfano wa sura ya wema wake. Ni mmoja, lakini aweza yote, na kwa kukaa katika yeye mwenyewe hufanya upya vyote; na tangu kizazi hadi kizazi, kwa kupita katika roho takatifu, huandaa rafiki za Mungu na manabii. Maana Mungu hampendi yeyote, isipokuwa yule aishiye pamoja na Hekima. Kwani yeye ni mzuri zaidi kuliko jua, na kuliko makundi yote ya nyota. Akilinganishwa na mwanga anaonekana kuwa anauzidi; maana baada ya mwanga hufuata usiku, lakini uovu hauwezi kumshinda Hekima. Hekima hutanda toka pembe hii hata pembe hiyo ya ulimwengu, kwa nguvu; naye huviratibisha vitu vyote kwa wema.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 119:89, 90, 91, 130, 135, 175
K. Neno lako, ee Bwana, linadumu milele hata milele.
Neno lako, ee Bwana, ni la milele;
limesimikwa imara mbinguni. K.
Ukweli wako upo toka kizazi hata kizazi;
umeiweka dunia, nayo yadumu. K.
Kwa maagizo yako vinasimama imara hata leo,
kwa maana vitu vyote ni watumishi wako. K.
Ufafanuzi wa maneno yako huleta mwanga,
huwapa ufahamu wajinga. K.
Umwangazie mtumishi wako uso wako;
unifundishe kanuni zako. K.
Nafsi yangu iishivyo itakusifu.
Nayo hukumu yako inanipa msaada. K.
SHANGILIO LA INJILI
YOHANE 15:5
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi, asema Bwana. Adumuye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa matunda mengi.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 17:20—25
Wakati ule: Mafarisayo walimwuliza Yesu, "Ufalme wa Mungu utakuja lini?" Akawajibu, "Ujio wa ufalme wa Mungu hauna majira yake, wala haiwezekani kusema, 'Upo hapa,' au 'Uko kule.' Kwa maana ufalme wa Mungu uko miongoni mwenu." Akawaambia wafuasi, "Siku zitakuja mtakapokuwa na hamu ya kuona siku moja ya siku za Mwana wa Mtu, msiione. Watawaambia, 'Tazameni kule! Tazameni hapa!' Msiende, wala msifuate. Kwa maana kama nuru imulikavyo toka upeo wa uwingu hata upeo mwingine, ndivyo Mwana wa Mtu atakavyokuwa katika siku yake. Lakini kwanza yambidi kupatwa na mateso mengi na kukataliwa na kizazi hiki."
Injili ya Bwana.