SOMO 1
Hekima Ya Sulemani 1:1—7
Pendeni haki enyi mnaotawala katika dunia; myawaze mambo ya Bwana kwa wema, na mtafuteni kwa moyo mnyofu. Kwa sababu hupatikana nao wasiomjaribu, na huonekana nao wasiokosa kumwamini. Maana mawazo yaliyopotoka yawatenganisha watu na Mungu, na nguvu, ikijaribiwa, inawashutumu wapumbavu. Kwani katika roho ipangayo mabaya haitaingia hekima, wala haitakaa katika mwili uliotawaliwa na dhambi. Maana roho takatifu yenye maadili itaitoroka hila, na itaondokana na mawazo yasiyo na ufahamu; udhalimu ukikaribia, yenyewe itafukuzwa. Maana hekima ni roho rafiki ya watu, wala hatamwachilia anayekufuru hatia ya midomo yake; kwa sababu Mungu ni shahidi wa viuno vyake pia ni mwangalizi wa kweli wa moyo wake na anasikia maneno ya ulimi wake. Maana roho wa Bwana ameujaza ulimwengu; nayo inavifungamanisha vitu vyote ina ujuzi wa kila sauti.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 139:1—3, 4—6, 7—8, 9—10 (K. 24b)
K. Uniongoze, ee Bwana, katika njia ya uzima.
Ee Bwana, umenichunguza na kunijua.
Wewe wajua kukaa na kusimama kwangu;
wayafahamu mawazo yangu tokea mbali.
Wapima kwenda na kupumzika kwangu;
waangalia njia zangu zote. K.
Maana kabla neno halijatoka kwenye ulimi wangu,
kumbe, ee Bwana, umekwisha kulijua lote.
Nyuma na mbele umenizunguka,
umeweka mkono wako juu yangu.
Maarifa hayo ni ya ajabu mno kwangu;
yananipita, nashindwa kuyafahamu. K.
Niende wapi mbali na roho yako,
nikimbilie wapi na uso wako?
Nikipanda juu mbinguni, wewe upo.
Nikijilaza chini kuzimuni, wewe upo! K.
Ningetwaa mbawa za mapambazuko
na kutua mbali ng'ambo ya bahari,
hata huko mkono wako utaniongoza;
na mkono wako wa kuume utanishika. K.
SHANGILIO LA INJILI
WAFILIPI 2:15d, 16a
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mtang'aa kama nuru katika ulimwengu, mkilishikilia lile neno la uzima.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 17:1—6
Wakati ule: Yesu aliwaambia wanafunzi wake, "Kutokea makwazo hakuepukiki, lakini ole wake yeye ayaletaye. Yamfaa zaidi kufungiwa jiwe la kusagia shingoni mwake na kutoswa baharini kuliko kumkwaza mmojawapo wa wadogo hawa. Jihadharini! Kama ndugu yako akikosa, umwonye; akitubu, msamehe. Na kama akikukosea mara saba siku moja, akarudi kwako mara saba akisema, 'Nimekosa,' basi, umsamehe." Mitume wakamwambia Bwana, "Tuongezee imani." Bwana akasema, "Mngekuwa na imani kiasi cha punje ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, 'Ng'oka, kapandikizwe baharini,' nao ungewatii."
Injili ya Bwana.