SOMO 1
Hekima Ya Sulemani 6:12—16
Hekima hung'aa, na hana uchafu, naye hutazamwa kwa urahisi na wale wampendao, na kuonekana na wale wanaomtafuta. Katika kujijulisha, huwatangulia wanaomtamani. Aamkaye asubuhi mapema kwa ajili yake, hatataabika, maana atamkuta ameketi kama mlinzi wa milango yake. Kwa maana kutafakari kuhusu hekima ni ukamilifu wa busara; naye akeshaye kwa ajili yake atakuwa mara hana masumbuko; mwenyewe huzungukazunguka kuwatafuta wanaomstahili, naye atajidhihirisha kwao kwa wema katika njia zao, na katika kila wazo yu pamoja nao.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 63:2, 3—4, 5—6, 7—8 (K. 2b)
K. Roho yangu inakuonea kiu, ee Bwana, Mungu wangu.
Ee Mungu, Mungu wangu, ninakutafuta kwa dhati!
Roho yangu inakuonea kiu;
mwili wangu unakuonea shauku,
katika nchi kavu, yenye kiu, isiyo na maji. K.
Hivyo nilikutazama katika patakatifu,
nione enzi yako na utukufu wako.
Fadhili zako ni bora kuliko maisha;
kwa hiyo midomo yangu itakutukuza! K.
Nitakusifu pindi niishipo;
kwa jina lako nitaiinua mikono yangu.
Roho yangu itafurahi kama kwa kushiba mafuta na vinono,
kwa midomo ya furaha, kinywa changu kitakusifu! K.
Ninapokukumbuka kitandani mwangu,
vipindi vyote vya usiku ninakufikiria wewe.
Kwa maana umekuwa msaada wangu,
na uvulini mwa mbawa zako nitashangilia. K.
SOMO 2
1 Wathesalonike 4:13—18
Ndugu, hatupendi kuwaficha juu ya wale waliolala, msije mkaona uchungu kama wengine wasio na matumaini. Maana tukisadiki ya kuwa Yesu alikufa na amefufuka, itakuwa sawa kwa wanaolala katika Yesu. Mungu atawaongoza njia moja na yeye. Kwa neno la Bwana twawaambieni haya: sisi tulio bado wazima na kusalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hatutawatangulia wale waliolala. Kwa maana kutakaposikika amri na sauti ya malaika mkuu na parapanda ya Mungu, Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni. Hapo wafu waliomo katika Kristo watafufuka kwanza. Halafu sisi tulioachwa wazima tutarushwa pamoja nao mawinguni kumkuta Kristo angani. Hivyo tutakuwa daima na Bwana. Basi, mtulizane kwa maneno hayo.
Neno la Bwana.
SHANGILIO LA INJILI
MATHAYO 24:42a, 44
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Kesheni, muwe tayari, kwa kuwa Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoidhania.
W. Aleluya.
INJILI
Mathayo 25:1—13
Wakati ule: Yesu aliwaambia wafuasi wake mfano huu, "Ufalme wa mbingu umefanana na wanawali kumi. Hao walitwaa taa zao, wakatoka kumlaki bwana harusi. Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara. Wale wapumbavu walitwaa taa zao bila kuchukua akiba ya mafuta, bali wenye busara walichukua chupa za mafuta pamoja na taa zao. Bwana harusi alikawia, nao wote wakasinzia, wakalala usingizi. Lakini katikati ya usiku kulipigwa mbiu, 'Haya bwana harusi anakuja. Nendeni kumlaki.' Hapo wanawali wale wote wakaamka, wakatengeneza taa zao. Wapumbavu wakawaambia wenye busara, 'Mtugawie mafuta yenu, maana taa zetu zinazimika.' Lakini wenye busara wakawajibu, 'Sivyo, hayatatutosha sisi na ninyi. Afadhali nendeni dukani, mkajinunulie.' Nao walipokwenda kununua, bwana harusi akafika. Wale waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye harusini. Mlango ukafungwa. Mwisho wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, 'Bwana, Bwana, utufungulie.' Naye akajibu akisema, 'Amin, nawaambieni, siwajui ninyi.' Basi kesheni, kwa maana hamjui siku wala saa."
Injili ya Bwana.