SOMO 1
Warumi 16:3—9, 16, 22—27
Ndugu: Salamu zangu kwa Prisila na Akwila, watumishi wenzangu katika Kristo Yesu. Hao walihatarisha maisha yao kwa ajili yangu. Si mimi peke yangu ninayewashukuru, ni Makanisa yote ya watu wa mataifa pia yanayowashukuru. Salamu zangu kwa waamini wenye kukutana nyumbani mwao, kadhalika Epaeineto, mwenzangu mpendwa aliye limbuko la Asia kwa Kristo. Salamu zangu kwa Maria aliyesumbuka sana kwa ajili yenu. Salamu zangu kwa Androniko na Yunia, jamaa zangu waliofungwa gerezani pamoja nami. Hao wanajulikana sana miongoni mwa mitume, tena walikuwa Wakristo kabla yangu mimi. Salamu zangu kwa Ampliato, mwenzi wangu mpendwa katika Kristo. Salamu zangu kwa Urbano, mfanyakazi mwenzetu katika Kristo, na kwa Stakisi, mpendwa wangu. Msalimiane kwa busu takatifu. Makanisa yote ya Kristo yanawasalimu. Na mimi Tertio mwandishi wa barua hii, ninawasalimu katika Bwana. Anawasalimu Gayo, mwenye kunikaribisha mimi na Kanisa lote. Wasalimu Erasto, mweka hazina wa mji huu, tena ndugu Kwarto. Neema ya Kristo, Bwana wetu iwe nanyi nyote. Amina. Asifiwe mwenye enzi ya kuwaimarisha ninyi kadiri ya Injili yangu na tangazo la Yesu Kristo, pia kadiri ya ufunuo wa fumbo lile lililofichika tangu karne ya milele. Sasa lakini limefunuliwa kwa njia ya Maandiko ya manabii kama Mungu wa milele alivyotaka ili kuwaongoza mataifa yote wapate kuitii imani. Mungu mmoja mwenye hekima aheshimiwe na kusifiwa kwa njia ya Yesu Kristo, milele na milele. Amina.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 145:2—3, 4—5, 10—11 (K. tazama 1)
K. Nitalisifu jina lako daima, ee Mungu na Mfalme wangu.
Kila siku nitakusifu,
na kutukuza jina lako daima na milele.
Bwana ni mkuu, na wa kusifiwa sana,
wala ukuu wake hautambulikani. K.
Kizazi kwa kizazi kitayatukuza matendo yako,
na kutangaza matendo yako makuu.
Nitatafakari fahari ya utukufu wa adhama yako,
na matendo yako ya ajabu. K.
Kazi zako zote zinakutukuza, ee Bwana,
wachaji wako wanakusifu.
Wanautaja utukufu wa ufalme wako,
wanauhadithia uwezo wako. K.
SHANGILIO LA INJILI
2 Wakorintho 8:9
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Ingawa Bwana wetu Yesu Kristo alikuwa tajiri, alijifanya maskini kwa ajili yenu, ili ninyi mpate kutajirika kwa umaskini wake.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 16:9—15
Wakati ule: Yesu aliwaambia wanafunzi wake; "Jifanyieni urafiki kwa mali inayoharibika, ili mnapoishiwa wawapokee katika makao ya milele. Aliye mwaminifu kwa mambo madogo ni mwaminifu pia kwa mambo makubwa; kadhalika asiye mwaminifu kwa mambo madogo, si mwaminifu kwa mambo makubwa. Basi, kama ninyi si waaminifu kwa mali isiyo haki, nani atawakabidhi mali ya kweli? Na kama hamwi waaminifu kwa mali ya mwingine, nani atawapa yenu wenyewe? Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili, ama atamchukia wa kwanza na kumpenda wa pili au atamjali wa kwanza na kumdharau mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu na fedha." Mafarisayo, wenye uroho wa fedha, waliyasikia hayo yote, wakamfyonya. Yesu akawaambia, "Ninyi mnajionyesha kama waadilifu mbele ya watu, lakini Mungu ajua mioyo yenu; yaliyo makubwa kwa watu ni chukizo mbele ya Mungu."
Injili ya Bwana.