SOMO 1
Warumi 15:14—21
Ndugu zangu: Mimi binafsi nina hakika ya kuwa mmejaa hisani, tena mna maarifa tele hata mnaweza ninyi wenyewe kuonyana. Katika sehemu fulani za barua hii nimewaandikieni waziwazi ili kuwakumbusha mambo mengine. Nimefanya hayo kwa nguvu ya neema niliyojaliwa na Mungu, ili niwe mtumishi wa Kristo Yesu kwa watu wa mataifa, tena kuhani kwa kuitangaza habari njema ya Mungu, kusudi watu wa mataifa wapate kuwa sadaka inayokubaliwa na Mungu n kutakaswa n Roho Mtakatifu. Basi, katika Kristo Yesu naona fahari kuhusu kazi za Mungu. Kwa maana kuhusu kuwaongoza watu wa mataifa wamtii Mungu, nathubutu kutaja mambo yale tu aliyoyatenda Kristo mwenyewe kwa utumishi wangu kwa maneno na matendo, kwa nguvu ya ishara na miujiza, kwa uwezo wa Roho wa Mungu. Hivyo nilizizunguka nchi toka Yerusalemu mpaka Ilirikumu nimemaliza kutangaza Injili ya Kristo kila mahali. Hapo niliangalia nisiihubiri Injili mahali jina la Kristo lilipokwishajulikana, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine, ila kama ilivyoandikwa: "Wataona wale wasiotangaziwa bado neno juu yake, na wataelewa wale wasiosikia habari."
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 98:1, 2—3ab, 3cd—4 (K. tazama 2b)
K. Bwana ameudhihirisha wokovu wake mbele ya macho ya mataifa.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
kwa maana amefanya mambo ya ajabu.
Mkono wake wa kulia,
na mkono wake mtakatifu, umemletea ushindi. K.
Bwana ameujulisha ushindi wake,
mbele ya macho ya mataifa ameifunua haki yake.
Amekumbuka wema na uaminifu wake
kwa nyumba ya Israeli. K.
Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote;
pigeni kelele za furaha, imbeni zaburi. K.
SHANGILIO LA INJILI
1 YOHANE 2:5
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Alishikaye neno lake Kristo, upendo wa Mungu umekamilika ndani mwake.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 16:1—8
Wakati ule: Yesu aliwaambia wafuasi wake, "Tajiri mmoja alikuwa na karani naye alishtakiwa kwake kwamba anatapanya mali zake. Akamwita, akamwambia, 'Je, nasikia nini juu yako? Toa hesabu ya ukarani wako, kwa maana huwezi kuwa karani tena.' Karani huyo akasema moyoni mwake, 'Nifanyeje? Maana bwana wangu ananiachisha kazi ya ukarani. Kulima siwezi na kuomba kama maskini naona haya. Najua la kufanya, ili baada ya kutolewa katika ukarani, wanipokee nyumbani kwao.' Akawaita wadeni wake mmoja mmoja, akamwambia wa kwanza, 'Una deni gani kwa bwana wangu?' Naye akajibu, 'Mapipa mia ya mafuta.' Akamwambia, 'Twaa hati yako ya deni; kaa upesi, andika hamsini.' Kisha akamwambia mwingine, 'Nawe una deni gani?' Akasema, 'Mifuko mia ya ngano.' Akamwambia, 'Twaa hati yako ya deni, andika themanini.' Bwana akamsifu karani mdanganyifu kwa sababu alifanya werevu. Maana wana wa dunia hii huwa na busara, katika mahusiano yao, kuliko wana wa mwanga."
Injili ya Bwana.