SOMO 1
Ufunuo 7:2—4, 9—14
Mimi, Yohane, nilimwona malaika mwingine akipanda kutoka macheo ya jua na kuuchukua muhuri wa Mungu aliye hai. Akapaza sauti, akawaambia malaika wanne waliopewa kuidhuru nchi na bahari, "Msiidhuru nchi wala bahari wala miti mpaka tutakapokwisha kuwatia muhuri watumishi wa Mungu wetu katika mapaji ya nyuso zao." Nikasikia idadi ya waliotiwa muhuri ndio mia na arobaini na nne elfu wa makabila yote ya mataifa wana wa Israeli. Baada ya hao, nikauona umati mkubwa asioweza mtu kuuhesabu, watu wa kila taifa, kabila, ukoo na lugha. Walikuwa wamesimama mbele ya kiti cha enzi na mbele ya Mwanakondoo, wamevikwa mavazi meupe na kushika matawi ya mitende mikononi mwao. Wakashangilia kwa sauti kubwa na kusema: "Wokovu watoka kwa Mungu wetu anayeketi katika kiti cha enzi na kwa Mwanakondoo." Malaika wakakizunguka kiti cha enzi na wazee na wenye uhai wanne, wakaanguka kifudifudi mbele ya kiti cha enzi, wakamsujudia Mungu wakisema: "Amina! Sifa, utukufu, hekima na shukrani, heshima na enzi na nguvu zina Mungu wetu daima na milele. Amina." Mmojawapo wa wale wazee akaniuliza, "Je, hawa waliovikwa mavazi meupe ni nani, na wametoka wapi?" Nikamjibu, "Bwana wangu, wajua wewe." Akaniambia, "Hawa wanatoka katika dhulumu kubwa; wamefua mavazi yao na kuyafanya meupe katika damu ya Mwanakondoo."
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 24:1—2, 3—4ab, 5—6 (K. 6)
K. Hiki ni kizazi cha wenye kuutafuta uso wako, ee Mungu.
Nchi ni yake Bwana na vyote vinavyoijaza,
dunia yote na wakaaji waliomo.
Maana Mungu ameweka misingi yake juu ya bahari,
ameisimika juu ya mito ya maji. K.
Ni nani atakayeupanda mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama mahali pake patakatifu?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
asiyeuinua moyo wake kwa mambo ya miungu. K.
Huyo atapata baraka kwa Bwana,
na tuzo ya Mungu Mwokozi wake.
Hiki ni kizazi cha wenye kumtafuta,
cha wenye kuutafuta uso wako, ee Mungu wa Yakobo. K.
SOMO 2
1 Yohane 3:1—3
Wapendwa: Tazameni jinsi mapendo aliyotujalia Mungu Baba yalivyo makubwa. Tunaitwa watoto wa Mungu, na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. Wapendwa, sasa tu watoto wa Mungu; lakini hali yetu ya baadaye haijajulikana bado. Ila itakapojulikana, tunajua kwamba tutakuwa hali Moja na Yesu, kwa maana tutamwona kama alivyo. Kila aliye na matumaini katika yeye, anajitakasa awe mtakatifu kama yeye alivyo mtakatifu.
Neno la Bwana.
SHANGILIO LA INJILI
MATHAYO 11:28
K. Aleluya. W. Aleluya
K. Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mzigo, nami nitawapumzisha, asema Bwana.
W. Aleluya.
INJILI
Mathayo 5:1—12a
Wakati ule: Yesu, alipoyaona makundi ya watu, alipanda juu ya mlima, akaketi na wafuasi wake wakamjia. Naye akafumbua kinywa chake, akawafundisha akisema: “Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri walio na huzuni, maana hao watatulizwa. Heri walio wapole, maana hao watairithi nchi. heri walio na njaa na kiu ya uadilifu, maana hao watashibishwa. Heri walio na huruma, maana hao watapa huruma. Heri walio na moyo safi, maana hao watamwona Mungu. heri wapatanishi, maana wataitwa wana Mungu. heri wanaodhulumiwa kwa ajili ya haki, maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watu wakiwatukana na kuwadhulumu na kuwasingizia vibaya kwa uwongo kwa ajili yangu. Furahini, shangilieni, kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni.”
Injili ya Bwana.