SOMO 1.
Warumi 13:8—10
Ndugu: Msiwe na deni kwa mtu yeyote, isipokuwa deni la kupendana. Kwani mwenye kumpenda mwenzake ameitimiza sheria. Kwa maana amri hizi: "Usizini, usiue, usitamani," na amri nyingine zote zimo katika amri hii moja: "Umpende mwenzako kama unavyojipenda mwenyewe." Ampendaye mwenzake hamtendei mabaya. Basi, upendo ni utimilifu wa sheria.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 112:1b—2, 4—5, 9 (K. 5a)
K. Heri mtu mkarimu na mwenye kuwaazima wengine.
au: Aleluya.
Heri mtu yule amchaye Bwana,
anayependezwa sana na amri zake.
Wazao wake watakuwa wenye nguvu katika nchi,
kizazi cha wenye adili kitabarikiwa. K.
Mwanga hwatokea wenye adili gizani;
ni mpole, mwenye huruma na haki.
Mtu mwema ni mkarimu na hukopesha,
huyatengeneza mambo yake kwa haki. K.
Amegawanya, na kuwapa maskini;
uadilifu wake wakaa milele;
pembe yake itainuliwa juu katika utukufu. K.
SHANGILIO LA INJILI
1 PETRO 4:14
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Heri yenu mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo, ni dalili ya kuwa Roho wa Mungu yu nanyi.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 14:25—33
Wakati ule: Watu wengi sana walimfuata Yesu, naye akawageukia, akawaambia, "Mtu akija kwangu bila ya kuwachukia baba na mama yake, mke na watoto, ndugu zake, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mfuasi wangu. Mtu asiyechukua msalaba wake na kunifuata, hawezi kuwa mfuasi wangu. Nani kati yenu anayenuia kujenga mnara haketi kwanza na kuhesabu gharama kama mali yake yatosha kwa kuumaliza? Asije akaweka msingi, halafu akashindwa kumaliza, hata watu wote wanauona wakaanza kumcheka, wakisema, 'Mtu huyu alianza kujenga, akashindwa kumaliza.' Au mfalme gani anayetaka kwenda vitani apigane na mfalme mwingine, haketi kwanza na kufanya shauri, kama ataweza na askari elfu kumi kumshambulia yule anayemjia na askari elfu ishirini? Kama sivyo, anatuma ujumbe kwake, angali mbali bado, amwulize masharti ya amani. Vivyo hivyo kila mmoja wenu asiyeachana na mali yake yote aliyo nayo, hawezi kuwa mfuasi wangu."
Injili ya Bwana.