SOMO 1
Warumi 12:5—16a
Ndugu: Sisi tulio wengi ni mwili mmoja katika Kristo na kila mmoja ni kiungo kwa wenzake. Basi, tunavyo vipaji mbalimbali kadiri ya neema tuliyopewa. Mtu akiwa na kipaji cha unabii, usemi wake ulingane na imani. Mtu akiwa na kipaji cha utumishi, basi atumikie, na mwenye kipaji cha ualimu, aelimishe. Mwenye kipaji cha faraja, afariji. Mwenye kutoa kitu atoe kwa unyofu. Aliye msimamizi, afanye bidii. Mwenye kufanya matendo ya huruma, afanye kwa uchangamfu. Upendo usiwe na unafiki. Chukieni yaliyo maovu shikilieni yaliyo mema. Mpendane kwa upendo wa kindugu. Mshindane katika kuheshimiana. Msilegee katika bidii; mwashwe roho; mtumikieni Bwana. Furahini katika matumaini; muwe na subira katika matatizo; salini daima. Wasaidieni wateule wakiwa na shida; mpende kuwakaribisha wageni. Wabarikini wenye kuwadhulumu, wabarikini msiwalaani. Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wenye kulia. Mwungane katika nia moja. Musijikaridie makuu, bali mshirikiane na wanyonge.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 131:1, 2, 3
K. Ee Bwana, iweke roho yangu kwa amani pembeni mwako.
Ee Bwana, moyo wangu hauna kiburi,
wala macho yangu hayainuki.
Wala sikufuata mambo makubwa,
au yaliyo ya ajabu mno kwangu. K.
Bali, nimeituliza nafsi yangu na kuinyamazisha,
kama vile mtoto, aliyeachishwa kunyonya
kifuani mwa mama yake,
ndivyo ilivyo roho yangu ndani yangu. K.
Ewe Israeli, umtumainie Bwana,
tangu sasa na hata milele. K.
SHANGILIO LA INJILI
MATHAYO 11:28
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kuelemewa na mizigo, nami nitawapumzisha, asema Bwana.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 14:15—24
Wakati ule: Mtu mmoja aliyekaa mezani aliposikia hayo alimwambia Yesu, "Ana heri atakayehudhuria karamu katika ufalme wa Mungu." Akamjibu, "Mtu mmoja alifanya karamu kubwa, akaalika watu wengi. Saa ya kula ilipotimia, akamtuma mtumishi wake kuwatangazia wale waalikwa, 'Njooni, karamu ni tayari.' Hapo wote wakaanza kuomba radhi kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, 'Nimenunua shamba sharti niende kulitazama; nakuomba uniwie radhi.' Mwingine akasema, 'Nimenunua ng'ombe wa kulima jozi tano na ninakwenda kuwajaribu, nakuomba uniwie radhi.' Mwingine akasema, 'Nimeoa mke, kwa hivyo siwezi kuja.' Mtumishi akarudi, akampasha bwana wake habari. Hapo mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumishi wake, 'Nenda upesi katika barabara na vichochoro vya mji, uwaingize humu maskini, vilema, vipofu na viwete.' Kisha mtumishi akasema, 'Bwana, amri yako imetimizwa, lakini kuna nafasi bado.' Bwana akamwambia mtumishi, 'Nenda kwenye njia na vitongoji, ukawalazimishe watu waingie, nyumba yangu ipate kujaa. Maana nawaambieni ya kwamba, hakuna hata mmoja wa wale walioalikwa atakayeonja karamu yangu.'"
Injili ya Bwana.