SOMO 1
Warumi 11:29—36
Ndugu: Mungu akiwajalia watu neema zake na kuwaita, hajuti tena. Kama vile ninyi zamani mlivyomkaidi Mungu, sasa lakini mmesamehewa kutokana na ukaidi wao. Vivyo hivyo wale wamekaidi kwa ajili ya msamaha mliyojaliwa ninyi, ili sasa wao pia wasamehewe. Kwa maana Mungu amewatia wote katika ukaidi wao, ili awasamehe wote. Ee wingi wa utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazitambuliki, wala njia zake hazichunguziki. Kwa maana ni nani aliyeyajua mawazo ya Bwana? Au ni nani aliyekuwa mshauri wake? Au ni nani aliyempa kitu kwanza, apate kurudishiwa? Kwa maana vitu vyote vimetoka kwake, vipo kwa uwezo wake, vinarudi kwake. Utukufu una yeye milele. Amina.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 69:30—31, 33—34, 36—37 (K. 14c)
K. Kwa huruma yako kuu unisikilize, ee Mungu.
Nami, niliye mnyonge na mwenye uchungu,
Ee Mungu, wokovu wako unilinde.
Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo;
nitamtukuza kwa kumtolea shukrani. K.
Enyi wanyonge, tazameni, furahini;
enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe!
Maana Bwana huwasikia wahitaji,
wala hawadharau wafungwa wake. K.
Maana Mungu ataisalimisha Sioni,
ataijenga upya miji ya Yuda.
Watu watakaa humo, na kuwa wenyeji wake;
na wazao wa watumishi wake watairithi;
na wenye kulipenda jina lake watakaa humo. K.
SHANGILIO LA INJILI
YOHANE 8:31b—32
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mkidumu katika neno langu, mtakuwa wanafunzi wangu, na mtatambua yaliyo ya kweli, asema Bwana.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 14:12—14
Wakati ule: Yesu alimwambia yule mmoja wa Mafarisayo aliyemwalika, "Ufanyapo karamu kwa chakula cha mchana au jioni, usiwakaribishe rafiki zako, wasije wakakualika pia na kukulipa sawa kwa sawa. Bali unapofanya karamu, uwaite maskini, vilema, viwete na vipofu; nawe utakuwa na heri, kwa sababu hawana cha kukulipa. Kwa maana utalipwa katika ufufuko wa waadilifu."
Injili ya Bwana.