SOMO 1
Malaki 1:14b—2:2b, 8—10
Mimi ni Mfalme mkuu, asema Bwana wa majeshi, na jina langu ni la kutisha katika mataifa. Na sasa, enyi makuhani, amri hii yawaelekea ninyi: kama hamnisikilizi, na kama hamkubali moyoni kulitukuza jina langu, asema Bwana wa majeshi, mimi nitawapelekea ninyi maapizo. Lakini ninyi mmeacha njia sawa, mmekwaza watu wengi wasishike sheria. Mmeharibu agano langu na Lawi, asema Bwana wa majeshi. Kwa hiyo nimewafanya ninyi mdharauliwe na kuwa wanyonge mbele ya watu wote, kwa kuwa hamshiki njia zangu, bali mnawapendelea watu katika maamuzi yenu. Je, sisi wote hatuna baba mmoja? Naye aliyetuumba si Mungu mmoja tu? Kwanini basi tunadanganyana kila mmoja na mwenzake, tukivunja agano la baba zetu?
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 131:1, 2, 3
K. Itulize nafsi yangu katika amani, ee Bwana.
Ee Bwana, moyo wangu hauna kiburi;
wala macho yangu hayainuki.
Wala sikufuata mambo makubwa,
au yaliyo ya ajabu mno kwangu. K.
Bali, nimetuliza nafsi yangu, na kuinyamazisha,
kama vile mtoto aliyeachishwa kunyonya
kifuani mwa mama yake,
ndivyo ilivyo roho yangu ndani yangu. K.
Ewe Israeli, umtumainie Bwana
tangu sasa na hata milele. K.
SOMO 2
1 Wathesalonike 2:7b—9, 13
Ndugu zangu: Tuliishi kati yenu kwa upole na unyenyekevu kama mama mwenye kuwalea watoto wake. Hivyo tunawaelekeeni kwa hamu ya kuwashirikisha Injili ya Mungu na nafsi zetu pia, kwa sababu mmekuwa wapendwa wetu. Ndugu, mnakumbuka jinsi tulivyotaabika na kuvumilia mno kwa kufanya kazi, kusudi tusimtegemee mtu yeyote kwenu wakati wa kuwafundisha Injili ya Mungu. Pia hatuachi kumshukuru Mungu kwa sababu hii: Neno la Mungu mmelipokea kwa kutusikiliza sisi, lakini hamkulipokea kama neno la wanadamu, bali kama Injili ya Bwana. Nalo hufanya kazi ndani yenu ninyi mliosadiki.
Neno la Bwana.
SHANGILIO LA INJILI
MATHAYO 23:9b, 10b
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Baba yenu ni mmoja ndiye aliye mbinguni; na mwalimu wenu ni mmoja, ndiye Kristo.
W. Aleluya.
INJILI
Mathayo 23:1—12
Wakati ule: Yesu aliwafundisha umati na wafuasi wake akisema, "Katika kiti cha Musa wameketi Waandishi na Mafarisayo. Kwa hiyo fanyeni na kushika yote wawaambiayo. Lakini matendo yao msiyaige, kwa maana wanasema lakini hawafanyi hivyo. Hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani, lakini wenyewe hawataki kuisogeza hata kwa kidole. Matendo yao yote huyafanya ili kutazamwa na watu. Kwa hiyo hutanua hirizi na kuongeza matamvua. Wanapenda nafasi za kwanza karamuni na viti vya mbele katika masinagogi, pia kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu 'Rabbi.' Bali ninyi msiitwe "Rabbi," maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Wala msimwite mtu 'baba' duniani, maana Baba yenu ni mmoja ndiye aliye mbinguni. Wala msikubali kuitwa 'Waalimu' maana mwalimu wenu ni mmoja naye ndiye Kristo. Aliye mkubwa miongoni mwenu ni mtumishi wenu. Kila anayejikweza atanyenyekeshwa, na kila ajinyenyekeshaye atakwezwa."
Injili ya Bwana.