SOMO 1
Warumi 11:1—2a, 11—12, 25—29
Ndugu: Nauliza, je, Mungu amelikataa taifa lake? La, hasha! Mimi pia ni Mwisraeli, mzao wa Abrahamu, wa ukoo wa Benjamini. Mungu hakulikataa taifa lake alilochagua zamani. Sasa ninauliza: Je, wamejikwaa ili waanguke? La, hasha! Bali kwa kosa lao wokovu uwafikie watu wa mataifa ili kuchochea wivu wa Waisraeli. Sasa ikiwa kosa lao ni faida kwa dunia, na namba yao ndogo ni faida kwa watu wa mataifa, itakuwaje kwa namba yao kamili? Ndugu, sipendi mtegemee akili zenu tu bila kulijua fumbo hili, yaani sehemu ya Waisraeli itashikwa na ushupavu mpaka idadi kamili ya watu wa mataifa itakapokuwa imejiunga. Kisha Israeli yote itaokolewa kama ilivyoandikwa: "Mwokozi atakuja kutoka Sioni, atatenga kutokuamini katika Yakobo. Hili ndilo agano nifanyalo nao wakati nitakapowaondolea dhambi zao." Mintarafu Injili, wao ni adui wa Mungu kwa ajili yenu, mintarafu kuteuliwa kwao, wao ni wapendwa wa Mungu kwa ajili ya mababu. Kwa maana Mungu akiwajalia watu neema zake na kuwaita, hajui tena.
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 94:12—13a, 14—15, 17—18 (K. 14a)
K. Bwana hatawaacha watu wake.
Heri mtu yule unayemwadhibu, ee Bwana,
na kumfundisha kwa sheria yako;
upate kumstarehesha siku za mabaya. K.
Maana Bwana hutalitupa taifa lako,
wala hutauacha urithi wako.
Kwani hukumu itakuwa tena ya haki;
na wote wenye moyo mnyofu wataifuata. K.
Kama Bwana asingalikuwa msaada wangu,
nafsi yangu ingalikaa upesi mahali pa kimya.
Niliposema, "Mguu wangu unateleza,"
fadhili zako, ee Bwana, zilinitegemeza. K.
SHANGILIO LA INJILI
MATHAYO 11:29ab
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mjitwike nira yangu, asema Bwana; na kujifunza kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo.
W. Aleluya.
INJILI
Luka 14:1, 7—11
Siku ya Sabato, [Yesu] aliingia nyumba ya mkubwa mmojawapo wa Mafarisayo ale chakula, nao wakawa wakimchunguza kwa makini. Akawaambia waalikwa mfano alipoona jinsi walivyojichagulia viti vya heshima. Labda mtu mwenye cheo kikubwa zaidi kuliko wewe amealikwa. Naye aliyewaalika wewe na yeye, asije akakuambia, 'Mpe nafasi huyu.' Hapo utaanza kuona aibu na kuketi mahali mwishoni. Bali, ukialikwa, nenda kakae mahali mwishoni, ili yule aliyekualika aje kukuambia, 'Rafiki, kaa mbele zaidi.' Hapo utapata heshima mbele ya wote wenye kukaa mezani pamoja nawe. Kwa maana kila ajikwezaye atashushwa, na kila ajishushaye atakwezwa."
Injili ya Bwana.