SOMO 1
Ayubu 19:23—27a
Ayubu, alijibu, "Ningetaka maneno yangu yaandikwe! Ningetaka yachorwe katika gombo, yachongwe milele katika mwamba kwa patasi ya chuma na kwa risasi! Mimi najua kwamba Mwokozi wangu anaishi, na kwamba atasimama juu ya mavumbi, yeye wa mwisho. Nami nikivikwa ngozi yangu, nitasimama wima, na katika mwili wangu nitamwona Mungu. Nami nitamwona mimi mwenyewe, wala si mwingine."
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 23:1—3, 3b—4, 5, 6
K. Hata nijapopita katika bonde la mauti, sitaogopa mabaya, kwani wewe upo pamoja nami.
Au: Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu.
Bwana ndiye mchungaji wangu,
sitapungukiwa na kitu.
Hunipumzisha katika malisho mabichi;
hunipeleka kwenye maji matulivu; hunipatia nguvu.
Huniongoza katika njia zilizo sawa
Kwa ajili ya jina lake. K.
Hata nijapopita katika bonde la giza,
siogopi mabaya, kwani wewe upo pamoja nami;
gongo lako na fimbo yako vyanituliza. K.
Waandaa meza mbele yangu,
machoni pa adui zangu;
umenipaka mafuta kichwani;
kikombe changu kinafurika. K.
Kweli, wema na fadhili zitanifuata
siku zote za maisha yangu.
Nitakaa nyumbani mwa Bwana
kwa miaka mingi ijayo. K.
SOMO 2
Warumi 5:5—11
Ndugu zangu: Kristo alikufa kwa ajili yetu wakati tulipokuwa bado dhaifu na mbali na Mungu. Kweli, ni vigumu mtu kufa kwa ajili ya mwadilifu. Labda yu tayari kutoa maisha yake kwa ajili ya mtu mwema. Hivyo Mungu amethibitisha mapendo yake atupendayo sisi kwa kufa kwake Kristo kwa ajili yetu tulipokuwa bado wakosefu. Lakini sasa baada ya kufanywa waadilifu kwa damu yake, tutazidi kuokolewa naye na hukumu ya Mungu. Basi, sisi tuliopatanishwa na Mungu kwa kifo cha mwanawe tulipokuwa bado adui zake, tutazidi baada ya kupatanishwa naye kusalimishwa kwa uzima wake. Zaidi ya hayo twajisifia Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo aliyekwisha kutupatia upatanisho.
Neno la Bwana.
SHANGILIO LA INJILI
TAZAMA MATHAYO 11:25
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Nakutukuza, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewafunulia watoto wachanga mafumbo ya ufalme.
W. Aleluya.
INJILI
Mathayo 5:1—12a
Wakati ule: Yesu, alipoyaona makundi ya watu, alipanda juu ya mlima, akaketi na wafuasi wake wakamjia. Naye akafumbua kinywa chake, akawafundisha akisema: “Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri walio na huzuni, maana hao watatulizwa. Heri walio wapole, maana hao watairithi nchi. heri walio na njaa na kiu ya uadilifu, maana hao watashibishwa. Heri walio na huruma, maana hao watapa huruma. Heri walio na moyo safi, maana hao watamwona Mungu. heri wapatanishi, maana wataitwa wana Mungu. heri wanaodhulumiwa kwa ajili ya haki, maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watu wakiwatukana na kuwadhulumu na kuwasingizia vibaya kwa uwongo kwa ajili yangu. Furahini, shangilieni, kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni.”
Injili ya Bwana.