KUMBUKUMBU YA WAT. MARTHA MARIA NA LAZARO, JULAI 29, 2024
RANGI YA KILITURJIA: NYEUPE 🤍
SOMO LA KWANZA
YEREMIA 13:1—11
Taifa hili litageuka kuwa kama mshipi huo, usiofaa tena kwa lolote.
Somo katika kitabu cha Nabii Yeremia
Bwana aliniambia hivi: "Nenda, ukajinunulie mshipi wa kitani; ukajivike kiunoni, wala usiutie kwenye maji. Basi nikanunua mshipi, kama Bwana alivyoniagiza, nikajivika kiunoní." Neno la Bwana likanifikia mara ya pili, likisema: "Twaa mshipi ule ulionunua, ulio kiunoni mwako, kisha simama uende kwenye mto Perathi, ukaufiche huko katika ufa wa mwamba." Basi nikaenda, nikauficha karibu na Mto Eufrate, kama Bwana alivyoniagiza. Ikawa, baada ya siku nyingi, Bwana akaniambia: "Inuka, uende kwenye Mto Eufrate, na huko uutwae tena ule mshipi, niliokuagiza kuuficha huko." Basi nikaenda kwenye Mto Eufrate, nikatafuta nikautwaa ule mshipi kutoka mahali nilipouficha. Lakini tazama, mshipi ule ulikuwa umeharibika, wala haukufaa tena kwa lolote! Hapo neno la Bwana likanifikia likisema: “Bwana amesema hivi: Jinsi hiyo hiyo nitaharibu kiburi cha Yuda, na kiburi kikuu cha Yerusalemu. Taifa hili ni baya, ni watu wanaokataa kusikiliza maneno yangu, ni watu wanaokwenda kwa kufuata ugumu wa moyo wao, wanaofuata miungu wengine na kuwatumikia na kuwaangukia. Taifa hili litageuka kuwa kama mshipi huo, usiofaa tena kwa lolote. Maana kama vile mshipi unavyoshikamana na kiuno cha mtu, ndivyo nilivyowafanyia nyumba yote ya Israeli na nyumba yote ya Yuda, wapate kushikamana nami asema Bwana, niliwafanya
wawe kwangu mimi taifa, na jina, na sifa, na mapambo. Lakini
wao hawakusikiliza.'
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
ZABURI YA KUITIKIZANA
KUMBUKUMBU 32:18—19, 20, 21
K. Umemsahau Mungu aliyekuumba.
Unamdharau mwamba aliyekuzaa, unamsahau Mungu aliyekuumba.
Bwana akaona, na kwa hasira yake
akawatupa wanawe na binti zake. K.
Akasema: Nitaficha uso wangu mbele yao,
nitaona yatakayowatukia mwisho,
kwa kuwa ni kizazi kipotovu,
wana wasio na uaminifu! K.
Wamenitia wivu kwa "kisicho Mungu,"
wamenikasirisha na vitu visivyo na maana,
basi, mimi nitawatia wivu kwa wasio watu,"
nitawakasirisha kwa taifa pumbavu. K.
SHANGILIO LA INJILI
YAKOBO 1:18
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Kwa hiari yake ametuzaa kwa neno la ukweli, tupate kuwa kama limbuko la viumbe vyake.
W. Aleluya.
SOMO LA INJILI
MATHAYO 13:31—35
Mbegu ya haradali huwa mti mkubwa kuliko mimea yote, hata ndege wa angani huja na kukaa katika matawi yake.
† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo
Wakati ule: Yesu aliwasimulia watu mfano mwingine akisema, "Ufalme wa mbingu umefanana na mbegu ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake. Nayo ni ndogo kuliko mbegu zote. Lakini ikiisha kumea huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata ndege wa angani huja na kukaa katika matawi yake." Akawaambia mfano mwingine: "Ufalme wambingu umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaichanganya na pishi tatu za unga, hata wote ukachacha." Hayo yote Yesu aliyasema kwa makundi ya watu kwa mifano. Pasipo mifano hakusema nao. Ilikuwa hivyo ili kitimie kile kilichosemwa na nabii, Nitafumbua kinywa changu kwa mifano, nitatangaza yaliyofichika tangu mwanzo wa dunia."
INJILI YA BWANA... SIFA KWAKO EE KRISTO