RANGI YA KILITURJIA: ZAMBARAU 💜
SOMO LA KWANZA
KUMBUKUMBU LA TORATI 4:1, 5—9
Zishike amri na kazi itakuwa kamili.
Somo katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati
Musa alinena na wana wa Israeli akisema, “Sasa Israeli, sikilizeni sheria na amri ninazowafundisha leo hivi ili mzishike kwa matendo, kusudi mpate kuishi na kuingia na kuitwaa nchi ile ambayo Bwana Mungu wa baba zenu amewapa. Angalieni, jinsi Bwana Mungu wangu alivyoniamuru, ndivyo ninavyowafunza sheria na amri ili mzishike kwa matendo katika nchi ambayo mnakwenda kuimiliki. Zishikeni na kutimiza kwa matendo, ndiyo hekima yenu na uelewa wenu machoni pa mataifa. Watakapojua sheria hizi zote, watasema, ‘Hakuna taifa jingine lenye hekima na utaratibu kama taifa hili kuu.’ Basi taifa jongine lipi lililo kubwa vile hata miungu yake inakaribia kama Bwana Mungu wetu akivyotukaribia sisi, kila tumwombapo? Taifa kubwa lipi hilo lililo na sheria na amri zake zenye haki kama Sheria hii yote ninayoiweka leo mbele yenu? Wewe lakini uwe macho usisahau mambo haya ambayo macho yako yaliona, wala usikubali yafutike hata siku moja ya maisha yako, yatoke moyoni mwako, bali uyafundishe watoto wako na wajukuu wako.”
NENO LA BWANA… TUMSHUKURU MUNGU.
ZABURI YA KUITIKIZANA
147:12—13, 15—16, 19—20 (K. 12a)
K. Eee Yerusalemu, umtukuze Bwana!
Umtukuze Bwana, ee Yerusalemu,
umsifu Mungu wako, ee Sioni.
Kwani alikaza komeo ya malango yako,
akawabariki wana wako ndani yako. K.
Huipeleka amri yake duniani, / neno lake lapiga mbio sana!
Hivyo huifanya theluji kama sufu,
na kutapanya jalidi kama majivu. K.
Hulitangaza neno lake kwa Yakobo,
nazo amri na kanuni zake kwa Israeli.
Hakulitendea taifa jingine lolote lile hayo,
Na wala amri kama hizo hawakuzijua. K.
SHANGILIO LA INJILI
TAZAMA YOHANE 6:63c, 68c
W. Sifa na utukufu, kwa ee Kristo.
K. Maneno yako, ee Bwana, ni roho tena ni uzima.
Wewe una maneno ya uzima wa milele.
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
INJILI
MATHAYO 5:17—19
Azishikaye na kuzifundisha amri zangu ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.
Somo la InjIli takatifu ilivyoandikwa na Mathayo
Wakati ule: Yesu aliwaambia wafuasi wake, “Msidhani nimekuja kuitengua sheria au manabii. Sikuja kuitengua, ila kuikamilisha. Amin, nawaambieni, mpaka mwisho wa mbingu na dunia, hefuri moja ijapo ndogo wala nukta moja ya sheria haitatoweka hata yote yatimie. Basi, avunjaye moja tu ya hizi amri zilizo ndogo na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo na wa mwisho katika ufalme wa mbinguni. Bali azishikaye na kuzifundisha ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.”
INJILI YA BWANA… SIFA KWAKO EE KRISTO