RANGI YA KILITURJIA: ZAMBARAU 💜
SOMO LA KWANZA
MIKA 7:14—15, 18—20
Atazitupa dhambi zetu zote katika kilindi cha bahari.
Somo katika kitabu cha Nabii Mika
Uwachunge watu wa taifa lako fimbo yako, na kundi dogo LA watu wa urithi wako, wanaokaa peke yao msituni katikati ya Karmeli, walishwe katika Bashani na Gileadi, kama vile siku za kale. Kama siku za kutoka kwako katika nchi ya Misri, utuonyeshe mambo ya ajabu. Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kuondoa uovu na kusamehe makosa ya wale wa urithi wako waliosalia? Ndiwe Mungu asiyeshika hasira yake daima, kwa maana unapendezwa kuwa mwema. Utatuonea huruma tena utayakanyaga makosa yetu tena, utazitupa dhambi zetu zote katika kilindi cha bahari. Utamwonyesha Yakobo uaminifu wako, na Abrahamu wema wako, uliyowaapia baba zetu, tangu siku za kale.
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 103:1—2, 3—4, 9-10, 11—12 (K. 8a)
K. Bwana ni mwenye huruma na neema.
Umsifu Bwana, ee roho yangu,
na yote yaliyo ndani yangu, yalisifu jina lake takatifu!
Umsifu Bwana, ee roho yangu,
wala usizisahau fadhili zake zote. K.
Yeye akusamehe dhambi zako zote,
anakuponya na magonjwa yako yote,
yeye anaukomboa uhai wako na kaburi,
anakuvika taji la fadhili na rehema. K.
Yeye haendelei daima kukaripia,
wala hadumishi hasira yake milele.
Hajatutendea kadiri ya dhambi zetu,
wala hajatupatiliza kadiri ya makosa yetu. K.
Maana kama vile mbingu zinavyoinuka juu ya nchi,
ndivyo huruma ilivyo kubwa juu ya wote wamchao.
Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. K.
SHANGILIO LA INJILI
LUKA 15:18
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
K. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa mbele ya Mungu na mbele yako.
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
INJILI
LUKA 15:1—3, 11—32
Huyo ndugu yako alikuwa amekufa, na amefufuka tena.
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Luka
Wakati ule: Watoza ushuru wote na wakosefu walimjia Yesu ili wapate kumsikia, lakini Mafarisayo na Waandishi wakanung'unika, wakisema, "Huyu huwapokea wakosefu na anakula nao." Akawaambia mfano huu, "Mtu mmoja alikuwa na wana wawili, mdogo akamwambia baba yake, 'Baba, nipe sehemu ya mali iliyo haki yangu.' Basi baba akawagawia mali. Baada ya siku si nyingi, mdogo huyo akakusanya vyote akaenda mbali ugenini alikotapanya mali yake kwa kuishi maisha ya uasherati. Alipomaliza vyote, njaa iliingia nchi ile, naye akaanza kupatwa na shida. Basi akaenda akajiunga na mwenyeji wa huko aliyemtuma shambani kwake kulisha nguruwe. Akatamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, lakini hakuna mtu aliyempa kitu. Akajifikiria, akasema, 'Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanakula na kusaza, nami ninakufa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, "Baba, nimekosa mbele ya mbingu na mbele yako. Sistahili kuitwa tena mwanao; unifanye kama mmoja wa watumishi wako.'" Basi akaondoka, akarudi kwa baba yake. Baba yake alimwona mbali, akamwonea huruma. Akamkimbilia, akamkumbatia, akambusu. Mwana akamwambia, 'Baba, nimekosa mbele ya Mungu na mbele yako; sistahili kuitwa tena mwana wako.' Lakini baba akawaambia watumishi wake, 'Upesi, leteni joho maridadi, mkamvike, mtieni pete kidoleni na viatu miguuni. Tena mleteni ndama mnono, mkamchinje. Kisha tule na kufanya sherehe, kwa maana huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.' Kisha wakaanza kufanya shangwe. Sasa mzaliwa wake wa kwanza alikuwa bado shambani, na aliporudi na kuikaribia nyumba, alisikia vifijo na ngoma. Akamwita mmoja wa watumishi, akamwuliza, 'Kuna nini?' Naye akamwambia, 'Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama mnono, kwa sababu amempata salama.' Akakasirika, na alipokataa kuingia nyumbani, baba yake alitoka nje na kumsihi. Akamjibu baba yake, 'Tazama, miaka mingapi nimekutumikia, tena sijavunja amri yako hata mara moja; lakini hujanipa hata mwanambuzi nifanye tafrija pamoja na rafiki zangu. Lakini huyu mwana wako aliyekula mali yako pamoja na makahaba, aliporudi umemchinjia mara ndama mnono.' Akamjibu, 'Mwanangu, wewe umekuwa pamoja nami siku zote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Lakini sharti tufanye shangwe na furaha, kwa maana huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka tena; alikuwa amepotea, naye ameonekana.'"
INJILI YA BWANA... SIFA KWAKO EE KRISTO