RANGI YA KILITURJIA: KIJANI KIBICHI 💚
SOMO LA KWANZA
1 WAFALME 3:4—13
Mpatie mtumishi wako moyo wa hekima nipate kuwatawala watu wako.
Somo katika kitabu cha kwanza cha Wafalme
Wakati ule: Mfalme Sulemani alikwenda Gibeoni kutolea dhabihu pale,kwa sababu ndipo sehemu ya kuabudia ya mlimani palipokuwa maarufu zaidi. Hapo Sulemani alitoa sadaka elfu za kuteketezwa juu ya madhabahu ile. Na hapo Gibeoni, Bwana alimtokea Sulemani katika ndoto. Mungu akamwambia: Omba kitu utakacho nikupe. Sulemani akajibu, "Umemtendea mtumwa wako Daudi, baba yangu kwa upendeleo mkubwa, kwa kuwa alienenda vema mbele zako katika kweli, na haki na katika unyofu wa moyo; na umeendelea kuonyesha fadhili hii kubwa, kwa kumjalia mwana wa kuketi katika kiti chake kama ilivyo sasa. Na sasa, ee Bwana Mungu wangu, umenifanya mimi mtumishi wako kuwa mfalme mahali pa Daudi baba yangu; ila mimi ni kijana tu, sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia. Naye mtumishi wako yupo katikati ya taifa lako uliloliteua, taifa la watu wengi wasioweza kuhesabika, wala jumla yao kufahamiwa kwa sababu ni wengi mno. Basi umpe mtumishi wako moyo wa hekima nipate kuwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya. Maana ni nani awezaye kuwatawala hawa watu wako walio wengi hivi?" Bwana akapendezwa na ombi hili la Sulemani. Mungu akamwambia: "Kwa kuwa umeomba jambo hili — wala hukujitakia maisha marefu, wala hukujitakia utajiri, wala hukuomba roho za adui zako — bali umeomba hekima ya kujua kuhukumu — basi, tazama, ninatenda kama ulivyosema. Ninakupa moyo wa hekima na akili, hata kabla yako hakupatikana mtu kama wewe, na wala baada yako hatainuka mtu kama wewe. Hata mambo yale usiyoyaomba nimekupatia: utajiri, heshima na utukufu kushinda wafalme wengine wote.
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 119:9, 20, 11, 12, 13, 14 (K. 12b)
K. Unifundishe amri zako, ee Bwana.
Kijana atatunzaje njia yake iwe safi?
Kwa kulishika neno lako. K.
Nimekutafuta kwa moyo wangu wote;
usikubali niyaache maagizo yako. K.
Nimeweka neno lako moyoni mwangu,
nisije nikakutenda dhambi. K.
Usifiwe, ee Bwana;
unifundishe kanuni zako. K.
Kwa midomo yangu nimeyasimulia
mashauri yote ya kinywa chako. K.
Nimefurahia njia ya mafundisho yako
kama kwamba ni utajiri mkubwa. K.
SHANGILIO LA INJILI
YOHANE 10:27
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Kondoo wangu huisikia sauti yangu, asema Bwana; nami nawajua, nao wanifuata.
W. Aleluya.
INJILI
MARKO 6:30—34
Walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji.
†Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
Wakati ule: Mitume walikusanyika kwa Yesu na wakamweleza yote waliyoyafanya, na waliyoyafundisha. Akawaambia, "Njoni, twende sehemu ya upweke mpate kupumzika kidogo." Kwa maana watu waliokuja na kutoka walikuwa wengi mno hata wasipate nafasi ya kula. Wakaondoka kwa chombo waende mahali pa ukiwa, wao peke yao. Watu waliwaona wakiondoka, na wengi walitambua shabaha yao. Wakaenda hima kwa miguu toka miji yote, wakawatangulia kufika. Aliposhuka pwani, aliona umati mkubwa wa watu. Akawahurumia, kwa maana walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mengi.
INJILI YA BWANA... SIFA KWAKO EE KRISTO