SOMO LA KWANZA
2 Samueli 1:1—4, 11—12, 29, 23—27
Mwanzo wa kitabu cha pili cha Samueli
Siku zile: Daudi aliporudi kutoka kuwashinda Waamaleki, alikaa siku mbili huko Siklagi. Hata siku ya tatu akaja mtu mmoja kutoka kambi ya Sauli, nguo zake zikiwa zimeraruliwa, na kichwa chake kimejaa vumbi. Mtu huyo alipomfikia Daudi alijitupa chini, akamsujudia. Daudi akamwuliza, "Umetoka wapi wewe?" Akamjibu, "Nimetoroka kutoka katika kambi ya Waisraeli." Daudi akamwambia, "Tafadhali niambie, mambo yalikwendaje? Naye akamjibu, "Imetukia ya kuwa watu wamekimbia vitani, na kati yao wengi wameangamia, wakiwemo Sauli na Yonathani mwanaye." Ndipo Daudi akayashika na kuyararua mavazi yake, pamoja na watu wote waliokuwa pamoja naye. Waliomboleza na kulia na kufunga hadi jioni kwa ajili ya Sauli, na Yonathani na jeshi lote la Bwana, kwa sababu wameanguka kwa upanga. Kisha Daudi akaimba: "Ole! Fahari ya Israeli, Sauli, ameuawa juu ya vilima vyako; jinsi gani mashujaa wameanguka! Sauli na Yonathani, wapendwa waliopendeza, maishani wala mautini hawakutengana, walikuwa wepesi kuliko tai, na wenye nguvu kuliko simba! Enyi binti za Israeli, mlilieni Sauli, aliyewavika zambarau ya gharama, na kuyapamba kwa johari na dhahabu mavazi yenu. Looh! Wameangukaje mashujaa wa vita kwenye makali ya vita wameuawa mahali palipoinuka! Nimesikitika kwa ajili yako, Yonathani ndugu yangu! Ulikuwa rafiki wa dhati kwangu; upendo wako kwangu ulikuwa wa thamani kupita upendo wa wanawake. Jinsi gani mashujaa wameanguka, na silaha za vita zimetoweka!"
Neno la Bwana.
ZABURI YA KUITIKIZANA
Zaburi 80:2—3, 5—7 (K. 4b)
K. Tuangazishe uso wako, ee Bwana, nasi tutaokoka.
Ewe mchungaji wa Israeli, utusikilize,
ulimwongoza Yosefu kama kundi la wanyama!
Uketiye juu ya makerubi ujionyeshe,
mbele ya Efraimu, Benjamini, na Manase.
Uamshe nguvu zako kuu, uje, utusaidie tuwe salama. K.
Ee Bwana wa majeshi, utakasirika mpaka lini,
dhidi ya sala za watu wako? Umewalisha kwa mkate wa machozi,
umewanywesha machozi kwa wingi.
Umetufanya kuwa kichekesho kwa majirani zetu;
nao adui zetu mimi wanatuzomea wao kwa wao. K.
SHANGILIO LA INJILI
Matendo Ya Mitume 16:14b
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Uifungue mioyo yetu, ee Bwana, tupate kuyasikiliza maneno ya Mwanao.
W. Aleluya.
INJILI
Marko 3:20—21
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko
Wakati ule: Yesu alikwenda nyumbani na wafuasi wake; na umati ulikusanyika tena, hata wasipate nafasi ya kula. Jamaa zake walipopata habari, walitoka ili wamkamate, maana walisema, "Amerukwa na akili."
Injili ya Bwana.